RC Tabora ataka ushirikiano majukumu ya kijamii

Wanafunzi wa Cha Utumishi wa Umma wakifanya usafi katika eneo la Hospitali ya Wilaya ya Tabora katika Maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano. Picha na Robert Kakwesi.

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amesema utaratibu wa kushirikisha majeshi, wanavyuo pamoja na watumishi wa Serikali katika majukumu yenye manufaa kwa jamii kuna faida.

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amesema utaratibu wa kushirikisha majeshi, wanavyuo pamoja na watumishi wa Serikali katika majukumu yenye manufaa kwa jamii kuna faida.

Katika hotuba yake iliyotolewa na Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Dk Yahaya Nawanda katika kusherehekea miaka 58 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya usafi hospitali ya Wilaya, amesema mjumuiko huo una mafunzo kwa kizazi cha vijana.

"Hapa tunawafundisha vijana wetu namna ya kuishi na kushirikiana na wengine katika ujenzi wa Taifa" amesema

Ameeleza kuwa kushirikiana kufanya kazi za kijamii kunadumisha kundugu, upendo na umoja katika jamii na kuhimiza jambo hilo liwe endelevu katika Mkoa wa Tabora.

 Meya wa Manispaa ya Tabora, Ramadhan Kapela ameagiza kuwekwa changarawe katika barabara ya kuingia kwenye hospitali hiyo ili wananchi na wagonjwa wasipate shida kutokana na kuwa na tope katika baadhi ya maeneo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora, Dk Peter Nyanja ameshukuru kwa ushirikiano katika kufanya usafi katika hospitali ya Wilaya ambayo tayari imeanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje.

Maadhimisho ya miaka 58 ya Muungano kwa Mkoa wa Tabora yamefanyika kwa kufanya usafi maeneo ya hospitali ya Wilaya ya Tabora ambayo imeanza kutoa huduma wiki chache zilizopita.