RC Tabora atoa maagizo kwa Dc Kihongosi

Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Kenani Kihongosi (kushoto) akiapa mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian. Picha na Robert Kakwesi.

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Dk Batilda Burian amemuagiza Mkuu mpya wa Wilaya ya Urambo, Kenani Kihongosi kufuatilia hali ya chakula wilayani humo akihofia wananchi  kuvuna na kuuza bila kuachia akiba.

Tabora. Mkuu wa Mkoa wa Tabora,Dk Batilda Burian amemuagiza Mkuu mpya wa Wilaya ya Urambo, Kenani Kihongosi kufuatilia hali ya chakula wilayani humo akihofia wananchi  kuvuna na kuuza bila kuachia akiba.

Akizungumza leo Alhamisi Mei 25, 2023 baada ya kumuapisha Kihongosi, Dk Burian amesema hatua hiyo itasaidia kuwaepusha wananchi na upungufu wa chakula.

"Nenda mkajadili hali ya chakula ili wananchi wasije baadaye wakapatwa na upungufu kwa vile pia chakula kinapelekwa nje,”amesema

Amemtaka DC huyo kwenda kufuatilia kama kuna mabadiliko kwa wakulima wa tumbaku kiuchumi kwa vile soko la zao hilo linaendelea mkoani humo.

Dk Burian amemtaka pia kuviangalia na kuvifuatilia kwa ukaribu vyama vya msingi ili viwanufaishe wanachama wake.

Katika hatua nyingine amemuonya kuwa wakazi wa Urambo hawapendi kupelekeshwa na kumtaka kuwafahamu na kuwaeleza jambo pasipo hasira na wao watamuelewa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Urambo, Kenani Kihongosi amemuahidi Dk Burian kutekeleza maagizo na maelekezo aliyompa na kwamba atafanya kazi kwa bidii kwa kushirikina na viongozi wenzake.

"Nitashirikiana na viongozi wenzangu katika wilaya pasipo ubaguzi wowote na maagizo uliyonipa nitayafuata"amesema