RC Tanga awatoa hofu wananchi kutoka Ngorongoro

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema mkoa huo upo tayari kuwapokea Watanzania waliokubali kuhama katika Hifadhi Tengefu ya Ngorongoro.

  

Handeni. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Adam Malima amesema mkoa huo upo tayari kuwapokea Watanzania waliokubali kuhama katika Hifadhi Tengefu ya Ngorongoro.

Amesema maandalizi yamekamilika na amewataka wananchi wa Wilaya ya Handeni kuwapa ushirikiano Watanzania hao.

"Niwatake wananchi wa Handeni pamoja na Viongozi wakuu wa Idara za Serikali kuhakikisha tunawapa ushirikiano wenzetu na tujione wenye bahati kupata wageni wenye neema," amesema Malima.

Aidha alitoa onyo na kusema wapuuzwe wanaoongea lugha za kibaguzi na kichochezi kwa kuwa suala hilo linafanyika kwa hiyari kwa ajili ya mustakabali wa maendeleo ya Taifa.

"Nawasikia mnasema ooh Wamasai wanakuja hii lugha haifai kutumia, wanaokuja ni Watanzania wenzetu maana sisi hatutambuani kwa makabila bali kwa Utanzania wetu na tuwape ushirikiano bila kuwabagua," amebainisha Malima.

"Niwahakikishie wageni, sisi watu wa Tanga tumefurahi na tunaona tunabahati kubwa na tunamshukuru Rais kwa uamuzi wake wa kuona Tanga inaweza kuwapokea wenzetu hawa na kuishi nao vizuri. Tupo tayari na muda si mrefu tunaelekea Msomera kuwapokea wageni " amesema Malima.