REA yawataka makandarasi kuzingatia mikataba

Wajumbe wa Bodi ya wakurugenzi ya REA, wakikagua miradi ya umeme kwa vijiji na Vitongoji mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Bodi ya wakurugenzi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imewataka makandaradi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kuzingatia matakwa ya mikataba yao na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.

Same. Bodi ya wakurugenzi ya Wakala wa Nishati vijijini (REA), imewataka wakandaradi wanaotekeleza miradi ya umeme vijijini kuzingatia matakwa ya mikataba yao na kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati.

Wakizungumza leo Septemba 12, kwa nyakati tofauti wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya REA kwa vijiji na vitongoji mkoani Kilimanjaro, wajumbe wa bodi hiyo wamesema wamebaini changamoto kadhaa hasa katika miradi ya awamu ya pili na ya tatu, ikiwemo kuchelewesha kwa miradi.

Mmoja wa wajumbe hao, Francis Songela amesema kumekuwepo na changamoto kwa baadhi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya Rea na kusema tayari bodi imetoa maelekezo kwa Tanesco na wasimamizi wa Rea kuwasimamia wakandarasi na kuhakikisha wanakamilisha miradi kwa wakati.

"Kilimanjaro tumeona miradi mbalimbali inayotekelezwa na wakandarasi mbalimbali, tumebaini changamoto kadhaa hasa katika miradi ya raundi ya pili na ya tatu, tumekaa na wataalamu wetu Tanesco na wakandarasi kuweza kuweka mikakati ya kuhakikisha kwamba kazi ambazo zimepangwa zinakamilika kama ilivyoainishwa kwenye mikataba," amesema Songela

Aidha amesema REA wamepokea Sh45 bilioni, kwa ajili ya kupeleka umeme katika vituo vya afya na sehemu za pampu za maji, lengo likiwa ni kupambana na magonjwa ya milipuko ikiwemo Uviko 19.

"Fedha hizi zinalenga kupeleka umeme katika vituo vya afya na sehemu za pampu za maji, miradi ambayo ina visima vya maji havina umeme viweze kuunganishwa na huduma za maji ziweze kuboreshwa pamoja na vituo vya afya," amesema.

Mkuu wa Wilaya ya Same, Edward Mpogolo amesema baadhi ya wakandarasi wanaotekeleza miradi ya Rea, wamekuwa changamoto, kutokana na kutoonekana maeneo ya mradi na kutaka kuongezwa nguvu katika usimamizi ili kutimiza malengo ya serikali ya kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia wananchi.

Kwa upande wake msimamizi wa Miradi  Kilimanjaro, Silvano Tongeni, amesema kwa Mkoa huo vijiji 11 ndivyo havina umeme huku vitongoji ambavyo havina huduma hiyo vikiwa 319 na kwamba wanaendelea kusimamia wakandarasi ili waweze kutekeleza miradi kwa wakati.