Repoa yataja maeneo matatu kuimarisha uchumi

Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa, Dk Donald Mmari akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam. 

Muktasari:

  • Repoa imependekeza kuimarishwa kwa sekta ya uzalishaji, mnyoyoro wa thamani wa kidunia na ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma, ili kuharakisha ukuaji wa uchumi endelevu na jumuishi nchini.

Dar es Salaam. Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa) imependekeza maeneo matatu yanayohitaji mabadiliko ya kimuundo ili kuharakisha ukuaji wa uchumi endelevu na jumuishi ikiwemo kuimarisha sekta ya uzalishaji.

Mbali na uzalishaji, maeneo mengine ni pamoja na mnyoyoro wa thamani wa kidunia na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma.

Kwa mujibu Repoa, utafiti umeonyesha kuwa uchumi unakua, lakini maeneo makubwa ya uzalishaji mfano viwanda yamebaki palepale kwa asilimia 8 katika kipindi cha miaka 29 tangu 1990 hadi 2019 sekta hiyo ikiwa na idadi ndogo ya watu walioajiriwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Repoa Dk Mmari  ameyasema hayo leo Novemba 6, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu warsha ya mwaka ya utafiti inayotarajiwa kufanyika Novemba 8 na 9 mwaka huu  iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Ofisi ya Rais Mipango, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na taasisi ya Gatsby Africa.

Amesema, “Kutokana na hali hii maeneo ya uzalishaji madini, viwanda, kilimo na utoaji huduma yanatakiwa kufanyiwa marekebisho ili kuharakisha uchumi endelevu na shirikishi wa nchi, sekta hii bado haijaajiri watu wengi.”

Dk Mmari amebainisha kuwa eneo lingine linalohitaji mabadiliko ya muundo ni mikakati ya kuimarisha ushirikishwaji mzuri katika minyororo ya thamani ya kimataifa na chaguzi za uhusiano wa kimkakati ili kuongeza ushindani wa mabadiliko katika kilimo, viwanda na sekta zingine.

Katika mkutano huo itazindua Mpango wake wa Utafiti wa miaka mitano kuhusu Mabadiliko ya Kimuundo na Mwelekeo wa Maendeleo nchini Tanzania ambapo watafiti mbalimbali barani Afrika wanatarajiwa kuhudhuria na kubadilishana uzoefu wa kile ambacho nchi inaweza kufanya ili kuharakisha ukuaji wa uchumi jumuishi.

Pamoja na hayo ni kuboresha ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi katika kuongeza kasi ya mchakato wa mageuzi ya kiuchumi.

Amesema katika kongamano hilo watawashirikisha watafiti na washirika wa maendeleo katika kujadili namna gani Tanzania inaweza kuongeza kasi ya kiuchumi na kujenga muundo ili ukuaji wa uchumi uhusishe wananchi wengi zaidi na kuhimili changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na mdororo wa uchumi duniani unaosababishwa na vita vya Urusi na Ukraine pamoja na Uviko 19.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Gatsby Africa Samweli Kilua amesema taasisi hiyo imeshiriki kuandaa warsha hiyo kwa sababu mabadiliko ya mfumo wa uchumi ni kazi tunayofanya hivyo ushiriki wetu una maana kwetu.

Kilua amesema zipo nchi ambazo zimefanikiwa kupitia mabadiliko ya muundo na kuharakisha uchumi, hivyo katika mkutano huo, watatoa tafiti mbalimbali kuhusu umuhimu wa ushirikiano wa sekta binafsi katika kuharakisha uchumi.