Rich Mavoko adai abiria U/Ndege wanakaa muda mrefu kupima Covid-19, Serikali yajibu

Rich Mavoko adai abiria U/Ndege wanakaa muda mrefu kupima Covid-19, Serikali yajibu

Muktasari:

  • Msanii wa Bongofleva, Richard Martin maarufu Rich Mavoko amedai abiria wanaowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) nchini Tanzania wakitokea mataifa mbalimbali wanachukua muda mrefu kupima, kulipia fedha na kupata majibu ya ugonjwa wa Covid-19.

Dar es Salaam. Msanii wa Bongofleva, Richard Martin maarufu Rich Mavoko amedai abiria wanaowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) nchini Tanzania wakitokea mataifa mbalimbali wanachukua muda mrefu kupima, kulipia fedha na kupata majibu ya ugonjwa wa Covid-19.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumamosi Mei 15, 2021 nje ya uwanja huo akitoka Afrika Kusini, Mavoko amesema hadi abiria anakamilisha taratibu zote anatumia saa mbili, na kuomba wanaotoa huduma hiyo kuongezwa ili shughuli hiyo ifanyike kwa muda mfupi.

Hata hivyo, meneja wa viwanja vya ndege wa Wizara ya Afya, Kakuru Remidius ameieleza Mwananchi Digital leo kuwa utaratibu uliowekwa hauchukui saa mbili hata kama ndege zilizoshusha abiria ni nyingi.

Amebainisha kuwa hatua anazotakiwa kupitia abiria akiwasili ni  kupimwa joto, kulipia fedha benki na kufanya kipimo husika akibainisha kuwa shughuli hiyo inafanyika kwa saa mbili.

“Kuna virusi aina mpya vilivyojibadilisha, kwenye mipaka inabidi tuwe wakali na makini, upimaji haukuwepo wengi wanaona ni kitu kipya na gharama na siyo sisi tu wenzetu Burundi wanachaji Dola 100 (za Marekani), si kweli kwamba wanatumia muda mrefu kwani kipimo chetu kinachukua dakika nne hadi 10 kinatoa majibu,” amesema Remidius.

Katika maelezo yake kwa wanahabari leo, Mavoko anayetamba na wimbo wa Wa Moto amesema, “Nimefika hapa tangu saa nane mchana lakini nimejikuta natoka humo ndani ya uwanja saa 10 jioni  kwa sababu ya foleni ya kusubiri kupimwa ugonjwa huo.”

"Nashauri Serikali yetu pendwa iongeze basi walau watu wa kufanya kazi hiyo, kwa kuwa haipendezi mtu umetoka safari umechoka halafu unafika unaanza tena kusubiria foleni ndefu kutoka ndani. Nadhani hii pia inaweza kuwa sababu ya wengine wanaoishiwa uvumilivu kuanzisha vurugu ambazo zingeweza kuepukika.”

Licha ya kulalamika, msanii huyo ameipongeza Serikali kutokana na majibu kutoka haraka tofauti na nchi za Nigeria na Afrika Kusini alikodai kuwa majibu hutolewa saa 12 au 24 baada ya kupima.

Kuhusu muziki, amesema alikuwa Afrika Kusini kwa ajili ya kuandaa albamu yake ya kwanza anayotarajia kuiachia Juni, 2021 itakayokuwa na nyimbo 12  alizowashirikisha wasanii wa  Afrika Kusini na Nigeria pamoja na wasanii  wawili wa Tanzania.