Ridhiwani: Migogoro ya wafugaji inasababishwa na wavamizi

Ridhiwani: Migogoro ya wafugaji inasababishwa na wavamizi

Muktasari:

Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete amesema migogoro ya wafugaji inasababishwa na wavamizi na si wenyeji kama inavyodhaniwa na wengi.

Chalinze.  Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete amesema migogoro ya wafugaji inasababishwa na wavamizi na si wenyeji kama inavyodhaniwa na wengi.
Amesema wafugaji wavamizi ndio hufanya uharibifu wa miundombinu ya maji  kwa kuwa hawana maeneo ya malisho ya mifugo yao tofauti na wenyeji ambao wametengewa maeneo na halmashauri.
Ridhiwani ameeleza hayo alipokuwa anajadiliana na wataalamu wa mamlaka ya maji safi na maji taka (Dawasa) Chalinze  alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa maji wa Malandizi -Mboga unaofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa Sh17. 1 ambapo moja ya changamoto waliyotaja ni uharibifu wa miundombinu ya maji inayodhaniwa inafanywa na jamii ya wafugaji
“Ni kweli kuna uharibifu wa miundombinu ya maji..., kuna wakati nilifuatilia sana hii inakuaje nikabaini wanaohusika ni wafugaji wavamizi sio hawa wenyeji, kwa hiyo Dawasa  mnapofanya mikutano ya kuelimisha jamii umuhimu wa kutunza miundombinu ya maji mjue mnakutana na wale wenyeji na watakusikiliza tu.”
“Kisha nao watatumia nafasi hiyo  kuwaambia matatizo yao,  mfano wanataka kuongezewa maeneo ya kulishia mifugo lakini hawaombi kwa sababu wao ni sehemu ya wanaoharibu miundombinu, hapana wanataka sehemu ya kunywesha mifugo maji,” amesema Ridhiwani.
Awali, meneja wa Dawasa Chalinze,  Honest Makoi amesema wananchi wa eneo hilo wameanza kunufaika na huduma za maji, kwa sasa miradi miwili mikubwa inaendelea kutekelezwa ukiwemo ule wa awamu ya tatu wa Wami Chalinze na Mlandizi Mboga ambao utatoa maji kwenye mtambo wa mto Ruvu.
Amesema kwa sasa zaidi ya watu 270,000   wa Chalinze na  Morogoro wananufaika kwa kuongezewa upatikanaji wa maji.