RIPOTI MAALUMU: Minazi utajiri unaoelekea kutoweka nchini
Muktasari:
- Mnazi ni mti wa kipekee na unaweza kuingia katika orodha ya mazao machache duniani yenye maajabu.
Dar es Salaam. Kama kuna fursa ambayo Watanzania hawajaitilia maanani, ni pamoja na kilimo cha minazi.
Mnazi ni mti wa kipekee na unaweza kuingia katika orodha ya mazao machache duniani yenye maajabu.
Ndiyo maana wanaoujua hawakusita kuuita kuwa ni mti wa maisha, kwani karibu kila kitu chake ni mali.
Anzia mti wenyewe unaoweza kutumika kama mbao, tunda lake linalotoa mafuta, tui, maji, juisi. Bado hujazungumzia fursa nyingine chekwa kama machicha, makumbi, makuti, chelewa na majani. Ni fursa kuanzia fedha mfukoni hadi lishe mwilini!
Hata hivyo, kinachosikitisha ni kuwa zao hilo limo hatarini kutoweka, japo bado Tanzania inatajwa kushika nafasi ya 11 duniani katika uzalishaji wa zao hilo.
Kwa mujibu wa ripoti ya Worldatlas ya mwaka 2017, Tanzania ipo katika nafasi ya 11 ya nchi zinazozalisha nazi kwa wingi ambapo kwa mwaka huzalisha nazi zaidi ya 530,000. Ya kwanza ni Indonesia inayozalisha nazi 18.3 milioni..
Mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa zao hilo ni pamoja na Dar es Salaam, Pwani, Mtwara, Lindi, Tanga na Zanzibar.
Hata hivyo, hali ni tofauti katika mikoa hiyo kwa sasa kutokana na maeneo mengi ya uzalishaji wakulima kutotilia maanani mbinu bora za kilimo, mabadiliko ya tabianchi na hata mashamba kugeuzwa kuwa maeneo ya makazi.
Ongezeko la bei
Hivi karibuni zao la nazi limeonekana kupanda bei ambapo nazi moja kwa sasa inauzwa hadi Sh2500 kutoka Sh1,000 ya awali, huku zile za jumla zikifika kati ta Sh1,400 hadi Sh1,500 ambazo awali zilikuwa zikiuzwa kati ya Sh800 hadi Sh900.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, baadhi wafanyabiashara wanasema zipo sababu mbalimbali zilizochangia kupanda kwa zao hilo kubwa likiwa ukame.
“Nazi ni mmea kama mimea mingine inayohitaji mvua, hivyo kukosekana kwa mvua mwaka jana kulikosababisha ukame pia kumeathiri zao hili na kusababisha uzaaji wa nazi kuwa mdogo na hata nazi zake kuwa ndogo,” anasema Suleman Malulu mfanyabiashara wa nazi wilayani Mafia.
Yahaya Hassan anayeuza nazi katika soko la Ilala jijini Dar es Salaam kwa bei ya jumla, anasema uhaba huo wa nazi kwa sasa umesababisha nazi iliyokuwa inauzwa Sh300 sasa inauzwa Sh700 hadi Sh800 na ile iliyokuwa inauzwa Sh900 hadi inafika sokoni hapo anaiuza kati ya Sh1,200 hadi Sh1,300.
Athumani Ahmad, anasema kuongezeka kwa soko la nazi pia ni moja ya sababu ya zao hilo kuwa juu, ambapo kwa sasa hata ile mikoa ambayo walikuwa hawatumii nazi kupikia wanatumia na kubainisha kuwa hii ni kutokana na mwingiliano wa watu ambapo wanajifunza tamaduni za watu wengine ikiwemo mapishi.
“Mbali na kutumika kama kiungo, pia hutumika kwake kwenye kutengeneza bidhaa mbalimbali kumesababisha bei yake kupaa na kuwa adimu na hii inatokana minazi mingi ambayo tunakula kwa sasa ni ile ya enzi za ukoloni, kwani sio watu wengi wanafanya kilimo cha mazao hayo kama ilivyo mazao mengine.
Kwa upande wake, Amani Ngohengo, muuza mafuta ya nazi, anasema ni kutokana na kupanda kwa bei ya nazi hata mafuta yake yamepanda bei, ambapo yale ya kuchemsha yanayouzwa Sh20,000 kwa sasa kabla yalikuwa yakiuzwa kati ya Sh12,000 hadi Sh13,000 na ili upate lita moja itakulazimu kutumia nazi sio chini ya kumi.
Hassan Swalihu, anasema kumekuwepo na changamoto ya usafiri wa uhakika wa kusafirisha nazi hizo, kutokana na kutoeleweka kwa usafiri wa majini ambapo wao wanategemea zaidi kutumia mashua.
Kauli hii inaungwa mkono na Amri Haji, aliyesema mbali na usafiri wa uhakika lakini kumekuwepo na tozo nyingi katika kusafirisha zao hilo ambapo hadi lifike kwa mlaji wanakuwa wametumia gharama kubwa ukianzana ile ya mazao ya halmshauri ambayo ni Sh1600 kila gunia.
Haji akielezea kiundani gharama hizo, anasema gharama za kubeba kwa gari kutoa gunia moja shambani hadi bandarini ni Sh2,500 na unapofika bandarini unatakiwa ulipia mzigo pande zote mbili kwa bandari ya Mafia na bandari ya Nyamisati Sh1200 yaani Sh600 kila upande na kwa ajili ya chombo 3,000.
Hapo bado ushuru wa mazao 1500, gari kwa ajili ya kwenda sokoni Dar es Salaam, Sh 6000 kwa kila gunia, watu wa kubeba’makuli’ Sh1500 wilayani Mafia, ukifika Nyamisati Sh500, sokoni Dar Sh1000 na Sh500 kwa ajili ya ushuru wa soko.
Mmoja wa wananchi aliyejitambulisha kwa jina la Neema Kuzuro, anasema kuna haja ya Serikali kuwekeza katika kilimo cha nazi kama ilivyo kwa mazao mengine, na hii ni kutokana na kuwepo kwa mahitaji makubwa ya zao hilo kwa sasa ambapo aliitaka iwekeze kuanzia katika mbegu bora na zinazowezwa kuvunwa kwa muda mfupi.
“Kitaalamu nazi pindi inapopandwa hadi ianze kuja kuzaa inachukua kati ya miaka mitano hadi sita, lakini katika uvunaji unaweza kuvuna kwa miaka 40 hadi 50 na uvunaji wake ni kila baada ya miezi mitatu tangu ulipovuna.
Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mafia ambayo pia ni kinara wa uzalishaji wa zao hilo nchini, Juma Ally alisema kushuka kwa zao hilo kunachagizwa na mabadiliko ya tabia ya nchi na ukongwe wa minazi iliyokuwepo.
“Kimsingi, asilimia 90 ya minazi ambayo tunaitegemea kwa sasa imekuwepo kwa miongo kadhaa...Mbali na hilo, minazi tuliyonayo haiwezi kustahimili ukame na kama unavyojua, mabadiliko ya hali ya hewa ni tatizo kubwa,” alisema.
Kutokana na sababu hizo nazi sasa inauzwa kati ya Sh700 na Sh800 katika Kisiwa cha Mafia tofauti na mwaka mmoja uliopita ambapo iliuzwa kwa Sh400 na Sh300 kulingana na ukubwa.
“Kwa sasa, mkulima huvuna kati ya nazi tano hadi saba kwa kila mti kwa msimu, tofauti na misimu iliyopita ambapo mkulima alikuwa akivuna wastani wa nazi 25 hadi 30 kwa mti,” aliongeza.
Ili kuondokana na kadhia hii, Ally alisema kuna haja ya kuingizwa kwa aina mpya ya minazi ambayo itastahimili ukame na kuleta matokeo bora na yenye maslahi kwa mkulima.
Hali ni sawa pia kwa upande wa Zanzibar ambapo utafiti unaonyesha kuwa bei ya bidhaa hiyo imefikia Sh1,500 hadi Sh2,000. Sensa ya miti ya mwaka 2013/14 katika visiwa hivyo inaonyesha kuwa idadi ya minazi imepungua kutoka milioni 5.7 mwaka 1990 hadi milioni 3.4.
Mkakati wa Serikali
Akizungumza na Mwananchi, Meneja wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Mikocheni, Dk Fred Tairo anasema katika moja ya mikakati ya taasisi hiyo ni kulifufua zao la mnazi na tayari wametengewa bajeti yake ya takiribani Sh1 bilioni kwa mwaka ujao wa fedha.
Akilifafanua hilo, Dk Tairo anasema katika ufufuaji huo mbali ya kupeleka mbegu bora kwa wakulima, pia watawasambazia teknolojia ambazo waliwahi kuizindua miaka ya nyuma lakini walishindwa kuzifikisha kwao kutokana na kukosekana kwa fedha.’
“Mfano Lindi tulikuta mkulima anauza mafuta lita kwa Sh10, 000 kutokana na kutumia teknolojia duni, lakini mafuta hayohayo mjini yakikamuliwa kwa mashine nzuri yanauzwa Sh40,000,” anasema.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Exaud Kigahe, anasema katika mikakati ya kuhakikisha zao hili linatumika ipasavyo, wanaendelea kushawishi watu kutoka nje kuja kuwekeza viwanda hapa nchini vikiwemo vya mafuta ya kula kutokana na nchi kuwa na uhaba wa bidhaa hiyo.
Pamoja na kufanya hivyo, changamoto wanayoipata anasema ni wawekezaji kutopata malighafi za kutosha, jambo ambalo hawana majibu nalo ya haraka.
“Ni kutokana na hilo, hivi sasa tunapokutana na wawekezaji hao tumekuwa tukiwahamasisha kuingia kilimo cha mkataba na wakulima ili nao waone wanapolima wana soko la uhakika, kwa kuwa wengi walipuuza zao hilo hapo katikati kwani halikuangaliwa kama zao la biashara na hivyo wakulima kugeukia mazao mengine,”anasema Kigahe.
Baadhi ya viongozi wa Serikali katika maeneo yanayozalishwa nazi kwa wingi, wameweka wazi mikakati ya kukuza uzalishaji wa zao hilo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mafia, Kassim Ndumbo, anasema mojawapo ya mikakati katika zao hilo ni kuwahamasisha wakulima kusafisha mazao yao ikiwemo kupalilia, kwani kutokana na kuyatelekeza wamekuwa hawapati mavuno yanayostahili.
Pia amekuwa akikemea maofisa kilimo kukaa ofisini, badala yake akiwataka kwenda mashambani kutoa elimu kwa wakulima.
Mkurugenzi Halmashauri ya Kilwa, Eston Ngilangwa, anasema ni kweli zao hilo bado halijapewa kipaumbele licha ya kuwa na fursa nyingi.
Nazi mti wa maisha
Akizungumza katika mahojiano na Mwananchi, mtafiti mstaafu wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) Mikocheni Dk Zuberi Bira anasema nazi ni ‘Mti wa maisha’.
Anasema zao hilo lilipewa jina hilo kutokana na kuwa na matumizi mengi katika kila eneo lake kuanzia mti, majani hadi tunda lake.
Akielezea kuhusu historia yake anasema ni zao lililotoka nchi za Mashariki ya mbali na lililetwa na wafanyabiashara wa kikoloni wakiwemo Wareno na Waarabu, huku wengine wakiamini lilikuja kwa njia ya bahari kama uchafu mwingine unaotupwa baharini na ndio maana linaota zaidi katika mikoa ya Pwani.
Kwa hapa Tanzania anasema kuna aina tatu za mbegu ambazo hutumika ikiwemo minazi mirefu (East African Tall), minazi mifupi maarufu Kipemba (Red Dwarf) inayolimwa zaidi Pemba na chotara (Hybrid) ambayo ni mchanganyiko wa minazi mifupi na minazi mirefu.
Minazi mirefu tofauti yake ni kwamba ina kitako kifupi chini, inaanza kuzaa nazi ikiwa na miaka mitano hadi saba, inazaa nazi kubwa na huishi hadi miaka 75.
Wakati minazi mifupi, yenyewe ina kitako chembemba, huzaa kuanzia miaka miwili, inazaa nazi nyingi, lakini kuishi kwako sio miaka mingi kama ilivyo mirefu.
Dk Bira anawahamasisha watu kulima kwa wingi zao hili bila kuhofia muda wake mrefu kwa kuwa linaweza kulimwa na mazao ya muda mfupi kama miembe, michungwa, maharage, mahindi na mazao ya msimu.
Pia anasema uzuri wa zao hili haliitaji uangalizi wa karibu kama yalivyo mazao mengine na hivyo kukupa fursa ya kufanya shughuli nyingine za uzalishaji huku lenyewe likiendelea kumea.
“Wakati Tari inaendesha mradi wa zao la nazi miaka 25 iliyopita ambao ulikoma mwaka 2004 wakati huo ikijulikana kwa jina la National Coconut Development Program (NCDP) miaka ya 1985, Tanzania inaelezwa ilikuwa na minazi milioni 25 na ilikuwa ikiingizia nchi Sh1 bilioni kila mwaka na nyingi zilikuwa zikitumia kwa ajili ya matumizi ya nyumbani,” anasema Dk Bira.
Matumizi ya nazi
Nazi hutumika kama kiungo kinachoongeza ladha na harufu nzuri ya chakula.
Mafuta yake hutumika kupikia na kujipaka mwilini kama urembo na kama tiba kwani inakuelezwa kuwa ni kinga nzuri ya ngozi.
Unga lishe
Lilian Kaale, Mhadhiri Mwandamizi Idara ya Kilimo na Teknolojia ya Kilimo, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema unga wa machicha ya nazi ni mzuri katika kupikia uji, ugali, na vyakula vyote vya kuoka ikiwemo keki, maandazi, mkate, biskuti na skonzi na ni lishe nzuri kwa makuzi ya mtoto, wagonjwa na wazee na wajawazito kutokana na kuwa na virutubisho vingi ikiwemo madini ya chuma na Vitamini E.
“Kwa mfano kuna mtu anatakiwa kunywa uji wa unga wa mihogo tu kutokana na matatizo ya kiafya, lakini akichanganya na unga huu wa machicha ya nazi, hakika atakuwa ameuongezea virubisho,’’anasema.