Ripoti ya CAG yamuibua Mchengerwa
Muktasari:
- Asema ripoti imeonyesha Chuo cha Utumishi wa Umma kina mapato ambayo hayakupokewa yenye thamani ya Sh284.8 milioni
Dodoma. Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais) Menejimenti na Utumishi wa Umma, Mohamed Mchengerwa ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kufanyia kazi uchunguzi wa dosari za fedha katika taasisi zilizopo chini ya wizara hiyo zilizotajwa kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Mbali na kutoa agizo hilo, Mchengerwa ametaka majibu ya uchunguzi huo apewe Aprili 28 mwaka huu.
Mchengerwa alitoa agizo hilo juzi jioni wakati akijitambulisha kwa wafanyakazi wa wizara hiyo baada ya kuteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa waziri.
Alisema ripoti ya CAG ya ukaguzi wa Serikali kuu ya mwaka 2019/20, ilionyesha katika Chuo cha Utumishi wa Umma kuna mapato ambayo hayakupokewa yenye thamani ya Sh284.8 milioni na matumizi yasiyolipwa ya Sh2.301 bilioni.
Mchengerwa alisema katika ofisi ya Wakala wa Mafunzo ya kimataifa (Tagla) ripoti hiyo ilionyesha kuwapo kwa matumizi yasiyolipwa ya Sh645.3 milioni.
Mchengerwa alisema kuwa ofisi yake itatekeleza maagizo yote yalitolewa na Rais Samia, ikiwamo Takukuru kufanya uchunguzi wa upotevu wa fedha katika Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA).
Naibu waziri wa wizara hiyo, Deogratius Ndejembi alisema ili kujenga maadili kwa watumishi kuna haja ya kukitumia vyema chuo cha utumishi wa umma.
Alisema licha ya kuwa watumishi hao wamesoma kwenye vyuo vingine, lakini ni lazima wapikwe kwenye chuo hicho cha Serikali.