Rombo kupata taarifa za nchini
Godfrey Mramba, ambaye ni mtoto wa aliyekuwa waziri wa Fedha nchini Tanzania, Basil Pesambili Mramba akizungumza na vyombo vya habari mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph
Muktasari:
Mwingiliano wa masafa ya redio za nchi jirani ya Kenya na ndani ya nchi katika wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro kumemwibua mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Fedha nchini Tanzania, Godfrey Mramba na kufungua redio katika wilaya hiyo ambayo masafa yake hayaingiliani na masafa ya nchi nyingine ambapo amesema wilaya hiyo haitakuwa tena kama kisiwa.
Rombo. Mwingiliano wa masafa ya redio za nchi jirani ya Kenya na ndani ya nchi katika wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro kumemwibua mtoto wa aliyekuwa Waziri wa Fedha nchini Tanzania, Godfrey Mramba na kufungua redio katika wilaya hiyo ambayo masafa yake hayaingiliani na masafa ya nchi nyingine ambapo amesema wilaya hiyo haitakuwa tena kama kisiwa.
Redio Banana FM imewalenga wananchi wa Rombo ambao kwa miaka mingi wamekuwa wakisikiliza redio za Kenya pekee kutokana na changamoto ya mwingiliano wa mawasiliano yaliyopo katika wilaya hiyo.
Pamoja na kuanzishwa kwa redio hiyo sasa wananchi hao watapata matangazo ya moja kwa moja kutoka nchini Ujerumani baada ya redio hiyo kuunganisha matangazo yake na DW.
Akizungumza leo Jumapili Novemba 20, 2022 wakati wa uzinduzi wa ushirikiano wa redio Banana FM na DW ya nchini Ujerumani, Mkurugenzi wa redio hiyo, Godfrey Mramba amesema baada ya kuona kuna changamoto kubwa ya mwingiliano wa redio za Kenya wilayani humo na kwamba wananchi wa Rombo hawapati mawasiliano ya redio za ndani akalazimika kuanzisha redio hiyo kama mkombozi wa Warombo.
"Changamoto kubwa niliyoiona Rombo ni usikivu wa redio za ndani, Kabla ya kuanzisha redio hii wananchi Warombo walikuwa hawapati matangazo ya redio za Tanzania kwasababu redio nyingi zinazosikika Rombo ni za Kenya,"
"Niliona nifanye kitu ili sisi tusiwe kisiwa na tuwe sehemu ya jamii ya Watanzania, sasa Rombo sio kisiwa tena naomba wananchi watumie redio hii kwa namna ambavyo itawasaidia kiuchumi, kijamii pamoja na mambo mengine,"
Amesema wakati wa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 ilikuwa ni ngumu sana wananchi wa wilaya hiyo kupata taarifa sahihi juu ya ugonjwa huo kutokana na redio za Tanzania zilikuwa hazisikiki katika wilaya hiyo.
Naye Mwakilishi wa DW nchini Tanzania, Baltazar Kitundu amesema ushirikiano wa redio hiyo pamoja na DW utawapa fursa wananchi hao wa Rombo kupata taarifa mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
"Redio hii ni muhimu kuwepo kwa wakazi wa Rombo kwa Kuwa hata panapotokea majanga mbalimbali inakuwa rahisi taarifa kuwafikia kwa wakati na inakuwa ni tofauti na kukiwa hakuna redio kabisa,"amesema Kitundu
Akizungumzia umuhimu wa redio hiyo, mmoja wa wananchi wa Rombo, Adolfina Joseph amesema kwa miaka mingi wamekuwa wakisikiliza redio za Kenya kutokana na mwingiliano wa mawasiliano uliopo.
"Kwa miaka mingi tumekuwa tukisikiliza redio za Kenya ndio zinazosikika kirahisi huku, tunashukuru kusogezewa huduma hii ya redio maana kwa kweli ni shida sana kupata redio za ndani na hii inakuwa ni ngumu sana hata wakati mwingine kama taarifa muhimu zinazotolewa na serikali hatuzipati kwa wakati,"
Aggrey Tesha, mkazi wa Tarakea amesema redio hiyo ni mkombozi wa Warombo kwa kuwa eneo walilopo lipo mpakani mwa Kenya na Tanzania kwa hiyo ni vigumu redio za Tanzania kusikika katika maeneo hayo.
"Sio redio tuu hata mitandao ya simu ina ingiliana sana na ya Kenya kwa hiyo mtandao umekuwa ni wa shida hapa mpakani hivyo tunashukuru maboresho haya yanayofanywa na wadau wazalendo wa wilaya hii, pia tunaiomba serikali iendelee kuona umuhimu wa namna ya kutatua changamoto hizi za mwingiliano wa mawasiliano na nchi nyingine,"amesema Fedha