RPC Manyara ataja vifo vya watu wawili akiwemo mwanafunzi

Kamanda wa Polisi mkoa wa Manyara, RPC George Katabazi, athibitisha vifo vya watu wawili akiwemo mwanafunzi wa shule ya Sekondari Edward Ole Lekaita, Picha na Mohamed Hamad

Muktasari:

  • Mwili wa mwanaume waokotwa porini ukiwa hauna kichwa wala miguu.

Kiteto. Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara, RPC George Katabazi amethibitisha vifo vya watu wawili waliopoteza maisha akiwemo mwanafunzi wa shule ya sekondari Edward Ole Lekaita aliyekosa hewa akiwa amelala chumbani kwake.

Kamanda Katabazi amemtaja mwanafunzi huyo kuwa ni Philipo Simengo (16) alikuwa anasoma Shule ya Sekondari Edward Ole Lekaita kidato cha kwanza, kuwa usiku wa kuamkia Februari 9, 2023 alikutwa chumbani kwake alikopanga akiwa amepoteza maisha Kijiji cha Njiapanda, Kata ya Namelock.

Kwa mujibu wa kamanda Katabazi amesema mwanafunzi huyo alikuwa na wenzake hivyo baada ya kupika usiku huo waliagana kwenda kulala ambapo yeye alichukua jiko la moto na kwenda kulala nalo.

Alisema akiwa chumbani inaonekana alikosa hewa kwa kuwa hata hicho chumba chenyewe alichokuwa anaishi hakikuwa na dirisha, hali inayoonyesha kuwa alikosa hewa.

Aidha alisema marehemu huyo ni mwanafunzi wa shule hiyo mpya ya Edward Ole Lekaita iliyoanza mwaka 2023 kwamba alipoteza maisha akiwa ni tegemeo kati ya wanaofanya vizuri shuleni hapo.

Tukio lingine aliloeleza RPC Katabazi ni kukutwa kwa sehemu ya mwili wa mwanadamu ukiwa umetelekezwa porini ukiwa hauna kichwa wala miguu eneo la Kijiji cha Kimana Kata ya Partimbo.

"Jeshi la Polisi tulipata taarifa kwa raia mwema wa Kijiji cha Kimana kuwa kuna mwili umetelekezwa porini na baada ya kufika hapo tulibaini kuwa niĀ  mwanaume ukiwa hauna nguo, kichwa wala miguu," amesema.

Alisema hakuna mtu aliyeutambua mwili huo kwa kuwa uliharibika na hakuna mtu aliyeripoti kupotelewa na ndugu yake tangu zipatikane taarifa hizo.

Kamanda Katabazi ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari kuwa wanapolala wasiweke moto karibu na kitanda kwani kwa kufanya hivyo yanaweza kujitokeza madhara kama hayo mtu kupoteza maisha kwa kukosa hewa.

Kuhusu mwili wa aliyeokotwa Kijiji cha Kimana, RPC Katabazi ameonya tabia za baadhi ya watu kufanya uhalifu wa aina hiyo akisema Jeshi la Polisi linaendelea na msako wa kubaini waliofanya tukio hilo.