Rufaa ya Sabaya na wenzake – 5

Muktasari:

  • Mkanganyiko wa ushahidi kuhusu picha za CCTV zilizorekodiwa wawabeba Sabaya na wenzake

Mkanganyiko wa ushahidi kuhusu picha za CCTV zilizorekodiwa wawabeba Sabaya na wenzake

Katika sehemu ya nne tuliona jinsi Jaji Kisanya alivyojadili na mambo ya kuzingatia kabla ya hukumu baada ya kubaini ukiukwaji wa sheria katika mwenendo wa kesi ya msingi.

Moja ya mambo aliyoyabainisha ni dosari katika hati ya mashtaka jinsi ilivyokinzana na ushahidi pamoja na mkanganyiko wa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka, hususan ushahidi wa picha za CCTV. Fuatilia sehemu hii ya tano na ya mwisho.

Jaji Kisanya alibainisha kuwa moja ya mikanganyiko katika ushahidi ilijitokeza katika picha za usalama (CCTV) za dukani kwa mlalamikaji na shahidi wa kwanza wa mashtaka, Mohamed Saad.

Alisema kama ilivyobainishwa na mmoja wa mawakili wa Sabaya, Moses Mahuna, shahidi wa kwanza upande wa mashtaka katika ushahidi aliieleza mahakama kuwa matukio yote yalirekodiwa kamera ya CCTV.

Lakini vilevile katika ushahidi wake alisema “sikuwepo dukani wakati Sh2,769,000 zilipoibwa, sijui nani miongoni mwa washtakiwa aliniamuru kufika dukani ndani ya dakika tano. Yote yaliyotokea dukani niliyaona kwenye kamera ya CCTV.”

Wakati akihojiwa zaidi na mmoja wa mawakili wa utetezi, Olawa kuhusu CCTV kurekodi tukio, shahidi huyo alieleza kuwa, “nilielezwa na Numas (Justine Numas, mmoja wa wasimazi wa duka) kuwa washtakiwa waliiba Sh2,769,000. Kadhalika kamera ya CCTV inawaonesha hao waliochukua pesa.”

Jaji Kisanya baada ya kurejea sehemu za ushahidi huo anasema unakinzana na wa shahidi wa saba na wa 11.

Amebainisha kuwa wapelelezi hao katika ushahidi wao unaonyesha kuwa kamera za CCTV zilikuwa zimehujumiwa na kugeuziwa sehemu nyingine.

“Duka lilikuwa na kamera za CCTV, lakini kwa makusudi ili kwamba tukio lisiweze kurekodiwa, kamera nne zilikuwa zimegeuzwa kuelekea ukutani.”

Baada ya kurejea sehemu ya ushahidi wa mashahidi hao, Jaji Kisanya alisema ni dhahiri kwamba shahidi wa kwanza kwa upande mmoja na shahidi wa saba na wa 11 kwa upande mwingine walikinzana kuhusu iwapo tukio la wizi lilirekodiwa na kamera za CCTV.

Wakijibu hoja hizo, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmed Mtenga na wakili wa Serikali Baraka Mgaya walimuomba Jaji Kisanya asizingatie ushahidi wa shahidi wa saba kuwa kamera za CCTV zilikuwa zimeelekezwa katika kona nyingine tofauti.

“Inaonekana wakili Mwandamizi ananialika kuuona ushahidi wa footage za CCTV haukuwa na manufaa katika upelelezi,” alisema Jaji Kisanya.

Alisema kuwa kwa kuzingatia mazingira ya kesi hiyo ni mtazamo wake kwamba mkanganyiko huo hauwezi kuchukuliwa kwa wepesi kwa kuwa unakwenda kwenye mzizi wa kesi.

Amesema kuwa hata kama ikizingatiwa kwamba mrufani wa kwanza (Sabaya) alikiri kwenda dukani kwa shahidi wa kwanza, lakini alikana kutenda kosa na kwamba katika hali hiyo ushahidi uliochukuliwa kutoka kwenye picha za CCTV ungeweza kutoa mwanga zaidi kuhusu nini kilitokea dukani.

“Ni mtazamo wangu kwamba mkanganyiko katika suala la CCTV unaibua shaka katika kujenga kesi,” amesema Jaji Kisanya.

Mkanganyiko mwingine ni kuhusu muda na kiasi cha pesa na mali nyingine zinazodaiwa kuibwa dukani humo.

Katika hilo Jaji Kisanya amebainisha kuwa shahidi wa pili katika ushahidi wake alidai kuwa pesa, mashine ya EFD na simu vilichukuliwa wakati mtu mwingine ambaye alikuwa hajakamatwa kwa amri ya Sabaya alipokuwa ameondoka dukani humo.

Anamnukuu shahidi huyo kuwa “kiongozi alirudi dukani baada ya hapo, na alimwachia Abu Mansur, Anas, Mzee Salim, Bakari Msangi na mwanamke. Kiongozi baada ya kuwa amerudi aliamuru pingu iliyokuwa mikononi mwa Abuu Mansur na Bakari kufunguliwa, kwa kuwa walikuwa wamefungwa pingu moja.

“Walichukua nyaraka, mashine ya EFD, simu za mkononi vilivyokuwa mikononi mwa wale waliokuwa wamekamatwa.

“Sikuona walichokichukua kutoka kwenye kaunta bali vilivyokuwa mezani. Kwenye kaunta kulikuwa na droo mbili. Ya juu ilikuwa kwa ajili ya kutunza nyaraka na sarafu na ya chini ilitumika kuhifadhi pesa. Kwa siku hiyo droo ya chini ilikuwa na Sh2,769,000.”

Jaji Kisanya amesema hata hivyo shahidi wa sita na wa nne walitoa ushahidi unaoashiria kwamba mali ziliibwa wakati shahidi wa sita akiwemo dukani.

Ananukuu: “Wakati tulipobaki tu watu wanne, mbali na Jeneral (Sabaya) na watu wake. Harijini (shahidi wa nne, wa pili na mwanamke) na mimi.

“Halafu Jeneral aliamuru vitu vyote vilivyokuwa juu ya kaunta vikusanywe. Niliona watu wa Jeneral wakichukua mali zetu kwenye kaunta na wakaviweka kwenye bahasha, wakachukua mashine ya EFD na karatasi zake (risiti). Simu zetu ziliwekwa kwenye bahasha.”

Akiamua hoja hiyo, Jaji Kisanya amesema kuwa anakubaliana na kanuni kuwa hitilafu za kawaida haziwezi kuepukika na kwamba anakubaliana na wakili wa Serikali kuwa mazingira ya kesi hiyo yanaashiria kuwa mashahidi walikuwa katika hali ya vurugu.

Hata hivyo, amesema mkanganyiko huo unakwenda kwenye mzizi wa kesi na kwamba unaibua mashaka kama shahidi wa sita wa upande wa mashtaka aliwashuhudia warufani wakikusanya au wakichukua vitu kutoka katika kaunta ya duka la shahidi wa kwanza (Saad).

Jaji Kisanya amesisitiza kuwa mkanganyiko huo unatia mashaka kuaminika kwa shahidi wa pili, wa nne na wa sita ambao wanakanganyana kama shahidi wa sita alikuwepo wakati warufani wakichukua mali hizo.

Kuhusiana na kiasi cha pesa kilichoibwa, Jaji alisema kulingana na kumbukumbu za kesi hiyo, shahidi wa kwanza na wa pili walipishana, kama zilikuwa ni Sh2,769,000 kinachoonekana kwenye hati ya mashtaka kilikuwa kinajumuisha Sh1 milioni zilizodaiwa kubakia dukani siku ya tukio.

Akijibu malalamiko hayo, wakili wa Serikali, Mtenga alisema shahidi wa kwanza na wa pili hawakukinzana huku akirejea kumbukumbu za rufaa hiyo na kudai kuwa Sh2,769,000 zinajumuisha na Sh1 milioni.

Hata hivyo, Jaji Kisanya alisema alichunguza kumbukumbu za rufaa kuwa kiasi cha pesa zilizoibwa ni Sh2,769,000.

Alisema kuwa shahidi huyo alikuwa imara kwamba alikijua kiasi hicho kwa kuwa tukio hilo lilitokea mara tu baada ya kumaliza kuhesabu mapato ya mauzo.

“Hivyo shahidi wa pili aliendelea kutoa ushahidi kwamba mapato ya mauzo (Sh2,769,000) yalijumuisha Sh1 milioni zilizoachwa na shahidi wa kwanza.”

Anarejea sehemu ya ushahidi wa shahidi huyo wa pili ambapo Jaji Kisanya anamnukuu:

“Tarehe 17/02/2021, nilimuita Saad (shahidi wa kwanza) aliyenieleza kuwa aliacha Sh1 milioni dukani, kiasi ambacho alikichukulia kama mapato ya mauzo. Katika Sh2,769,000 kiasi hicho kilijumuishwa.”

Jaji Kisanya alifafanua zaidi kuwa kwa upande mwingine ingawa shahidi wa kwanza (Saad), alitoa ushahidi kwamba aliacha pesa dukani, alieleza akiwa chini ya kiapo kuwa hakujua jumla yake.

“Wakati naondoka dukani kwenda msikitini, niliacha kiasi cha pesa ambacho sikujua jumla yake halisi.”

Jaji Kisanya anaendelea kusisitiza kuwa mkanganyiko huo si mdogo na kwamba unakwenda kwenye mzizi wa kesi, yaani kama Sh2,769,000 ziliibwa kutoka dukani kwa Saad, kama ilivyoelezwa kwenye shtaka la kwanza.

Mkanganyiko mwingine kuhusu kuwatambua washtakiwa wakati wa gwaride la utambuzi.

Shahidi alieleza kwamba wakati wa gwaride hilo aliwatambua watu wawili, aliowataja kuwa ni Deogratias Peter na Daniel Bura.

Hata hivyo, katika ushahidi wa shahidi wa tisa na kielelezo cha pili, ilionyeshwa kwamba mtuhumiwa aliyetambuliwa na shahidi wa sita ni Daniel Laurent Bura na Deogratias Peter haonekani kwenye ushahidi wa shahidi wa tisa na kielelezo cha pili. “Kutokana na uchambuzi huo, ninakubaliana na rufaa hii kwa namna ambavyo imeonyesha hapa. Hatimaye mwenendo wa kesi ya msingi unabatilishwa, hatia dhidi ya warufani inatenguliwa na adhabu iliyotolewa kwao inatupiliwa mbali.

“Inaamuriwa kwamba Lengai Ole Sabaya, Sylvester Wenceslaus Nyegu na Daniel Gabriel Mbura waachiliwe kutoka gerezani isipokuwa kama wataendelea kushikiliwa kwa sababu nyinginezo halali.”