Rushwa yagharimu mapato ya Serikali

Muktasari:

  • Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) imesema kuwa matukio ya ubadhirifu na udanganyifu wa matumizi ya fedha yamekuwa yakiigharimu Serikali na taasisi binafsi zaidi ya asilimia tano ya mapato yao kila mwaka, hali inayokwamisha maendeleo.

Arusha. Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) imesema kuwa matukio ya ubadhirifu na udanganyifu wa matumizi ya fedha yamekuwa yakiigharimu Serikali na taasisi binafsi zaidi ya asilimia tano ya mapato yao kila mwaka, hali inayokwamisha maendeleo.

Hayo yamesemwa juzi na mchunguzi mkuu wa Takukuru nchini, Stephen Agwanda kwenye mkutano mkuu wa mwaka wa wataalamu wa upelelezi wa masuala ya ubadhirifu na rushwa (ACFE) unaoendelea jijini hapa.

Alisema kuwa katika ripoti ya uchunguzi ya mwaka 2022, wamebaini matukio ya ubadhirifu na udanganyifu yamekuwa yakiigharimu Serikali na taasisi fedha nyingi, ambazo zingetumika kuleta maendeleo.

Alisema kutokana na hali hiyo, wameunda timu ya wataalamu wa upelelezi watakaofanya kazi ya kubaini na kuzuia matukio hayo, kabla hayajatokea au kuleta madhara.

“Changamoto katika kushughulikia makosa haya ni watekelezaji kuficha ushahidi kitaalamu,” alisema.

Kwa upande wake rais wa ACFE, Stella Cosmas alisema kuwa matukio ya ubadhirifu, udanganyifu na rushwa yanaendelea kuwepo kutokana na wahusika kutotiwa hatiani kulingana na makosa yao, hali inayosababishwa na wapelelezi kukosa au kushindwa kupata ushahidi wa kutosha.

“Katika mkutano huu tunalenga kuwasaidia wataalamu wa upelelezi wa masuala ya ubadhirifu na rushwa kupata mbinu za kisasa za kupeleleza matukio haya, ili kuyaibua kabla hayajatokea au kuleta madhara kwenye taasisi wanazofanyia kazi,” alisema.

Kwa upande wake Ofisa ubora na vihatarishi kutoka mamlaka ya usimamizi wa bandari Tanzania (TPA), Gladness Msuya alisema kuwa mafunzo katika mkutano huo yamemsaidia kujua mbinu mpya na viashiria vya ufisadi na rushwa na namna ya kuvidhibiti kabla havijatokea.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa bodi ya udhibiti na mapambano dhidi ya rushwa Afrika, Charity Hanene alisema chama hicho chenye wanachama zaidi ya 19,000 kutoka nchi 125 kina makao yake makuu nchini Marekani.