Ruto asema anautaka upinzani Kenya

Rais mteule wa Kenya, William Ruto

Muktasari:

Rais mteule wa Kenya, William Ruto leo Jumatatu Agosti 15, 2022 amesema Serikali yake itaruhusu uwepo wa upinzani kwa ajili ya kuleta uwajibikaji na kukuza demokrasia

Nairobi. Rais mteule wa Kenya, William Ruto leo Jumatatu Agosti 15, 2022 amesema Serikali yake itaruhusu uwepo wa upinzani kwa ajili ya kuleta uwajibikaji na kukuza demokrasia

Kauli hiyo ameitoa muda mchache tangu akabidhiwe cheti cha ushindi uliotokana na kura zilizopigwa Agosti 9, 2022 katika uchaguzi mkuu ambapo amewaambia waandishi wa habari kuwa hajawahi kuamini hadithi za maridhiano

“Sijawahi kuamini kwenye hadithi za maridhiano na upinzani (handshakes) kwasababu naamini demokrasia, kwasababu ukiwa na serikali ambayo haina upinzani unaitengeneza serikali isiyowajibika kama kitu tulichokishuhudia miaka minne iliyopita,”amesema

“Badala ya Serikali kukosolewa na wapinzani sasa wapinzani wanakuwa wanaunga mkono masuala ya kiserikali, kitu ambacho sitakihitaji kwenye serikali yangu,”ameongeza.

Ruto amesema kuwa asubuhi ya leo Agosti 15, 2022 ameongea na mpinzani wake Raila Odinga na wakakubaliana kuheshimu matokeo yoyote yatakayotoka kwaajili ya kutunza amani ya nchi hiyo.

Amesema kuwa atakuwa na mazungumzo na Rais anayetoka madarakani Uhuru Kenyatta kwa siku ya kesho Agosti 16, 2022.

“Sijaongea na Uhuru Kenyatta ila nina uhakika tutakuwa na mazungumzo kwasababu mimi ni Rais mteule kwahiyo lazima kutakuwa na kukabidhiana madaraka,”amesema.