Ruto kutoka kuuza kuku hadi urais Kenya

What you need to know:

Ni dhana iliyojengeka katika maisha ya mwanadamu kuwa watu wenye maisha duni ni nadra kufanikiwa kushika nyadhifa za juu serikali, Dk William Ruto, kuruka kihunzi hicho.

Dar es Salaam. Dk William Samoei Ruto, ndiye Rais wa Kenya. Ni mfano wa maisha ya watoto wengi maskini Wakenya ambao hudhani umaskini wao hauwezi kuwafanya wawe viongozi au matajiri.

Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) ya Kenya ilimtangaza kuwa mshindi wa kinyang’anyiro cha Uchaguzi Mkuu, uliofanyika Agosti 9, 2022 akiwashinda wenzake ambao ni Raila Odinga (Azimio la Umoja), George Wajackoyah (Chama cha Roots) na David Waihiga (Chama cha Agano).

Dk Ruto, amepenya kwenye ushindani mkali kutoka kwa Odinga kwa kupata kura milioni 7.1 dhidi ya kura milioni 6.9 za Odinga

Historia ya maisha yake ndiyo iliyochangia kwa kwa kiasi kikubwa kupata uungwaji wa mkono kutoka kwa Wakenya hususan wale wa kipato cha chini kupitia kauli mbiu yake ya ‘Taifa la wahangaikaji’. Alionekana ni mwenzao mwenye lengo la kuwakomboa kiuchumi.

Maisha yake yalianzia kwa kuuza kuku na karanga kando ya barabara katika maeneo ya kijijini kwao katika Mkoa wa Bonde la Ufa (Rift Valley).

Kwa hiyo sio jambo la kushangaza kwamba anajielezea kama kiongozi wa maskini wakati anapogombea kiti cha urais katika uchaguzi uliofanyika Agosti 9, 2022.

Alionekana kuungwa mkono zaidi na vijana ambao ukosefu wa ajira miongoni mwao ni takriban asilimia 40 huku uchumi wa nchi hiyo, ukielezewa kutotoa ajira za kutosha kuwaajiri vijana 800,000 wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka.

Alivyoingia katika siasa

Alijiunga na siasa katika mwaka 1992, ambapo alifunzwa na aliyekuwa Rais wa Kenya wakati huo Daniel Arap Moi.

Dk Ruto alikuwa sehemu ya tawi la vijana la chama kilichotawala wakati mmoja cha Moi na alikuwa mmoja wa wanaharakati waliopewa jukumu la kuhamasisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi katika mwaka huo huo.

Kwa sasa ana sifa ya kuwa mzungumzaji mwenye mamlaka mwenye uwezo wa kukusanya umati mkubwa katika mikutano ya kisiasa na mwenye kufanya vyema katika mahojiano na vyombo vya habari.

Mara nyingi huanza kuzungumza kwa kusema “Rafiki yangu”, matamshi yanayomsaidia kuanzisha uhusiano na wapiga kura.

Kuhama miungano

Baada ya kushikilia nyadhifa mbali mbali za uwaziri hadi kuwa Naibu wa Rais baada ya uchaguzi wa mwaka 2013.

Dk Ruto aligombea uchaguzi huo kama mgombea mwenza wa Rais anayeondoka madarakani Uhuru Kenyatta, ambapo aliwashangaza Wakenya wengi kwasababu walikuwa katika pande zinazopingana kisiasa katika uchaguzi uliotangulia.

Ulikuwa ni muungano wa manufaa, kwani wote wawili walikuwa wameshtakiwa na mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kwa Makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu baada ya kushtumiwa kuchochea ghasia baada ya uchaguzi wa mwaka 2007 ulioibua mgawanyiko mkubwa, ambapo watu 1,200 waliuawa.

Katika uchaguzi huo, Dk Ruto alikuwa ameunga mkono mgombea wa upinzani Raila Odinga-ambaye sasa ni hasimu wake kisiasa-huku Kenyatta akimuunga mkono aliyekuwa Rais wakati huo, Mwai Kibaki katika azma ya kuwania tena urais.

Muungano wao, uliopachikwa jina la ‘’bromance’’, ulizaa matunda kwani wanaume hao wawili walichukua mamlaka.

This page might use cookies if your analytics vendor requires them.