Saa 36 tamu, chungu za Kamala Harris

Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris akiagana na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango katika Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jijini Dar es Salaam jana. Picha na Ericky Boniphace
Dar es Salaam. Saa 36 za Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris hapa nchini zimekuwa za tofauti hasa katika Jiji la Dar es Salaam, ambalo wakati wa uwepo wake, baadhi wakisema kilikuwa kipindi cha usumbufu kwao huku wengine ikiwa neema.
Harris aliwasili nchini Machi 29, saa tano usiku akitokea Ghana ambako alianzia ziara yake ya kwanza katika bara la Afrika.
Licha ya umuhimu wa ziara ya kiongozi huyo wa juu wa Marekani kuonesha matunda ya kidiplomasia, kiuchumi na maeneo mengine ya ushirikiano kati ya nchi hizo, uwepo wake umesababisha usumbufu kwa baadhi ya watu, hasa watumiaji wa barabara kwani mambo yalikuwa tofauti kabisa.
Ulinzi uliimarishwa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na barabara zote zinazopita katika Hoteli ya Hyatt ambayo ndiyo aliyofikia, zilifungwa isipokuwa barabara ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT).
Wafanyabiashara wa samaki ambao huwa wanakwenda soko la samaki la Kivukoni, walilazimika kutembea kwa miguu baada ya kushushwa na daladala kwa sababu ya kufungwa kwa barabara ya Kivukoni.
“Sijui huu ugeni utaondoka lini, leo tumepata shida sana. Tunatembea na jua lote hili, bado natakiwa kurudi na mzigo wangu wa samaki, sijui nabebaje na magari hayapo,” alisema mfanyabiashara mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Ramadhan.
Juzi asubuhi, baadhi ya barabara zilifungwa na wananchi kuelekezwa kutumia njia mbadala ili kuepusha mwingiliano wa msafara wake ambao ulikuwa na zaidi ya magari 15.
Hali hiyo ilisababisha wengine kulalamika kuchelewa kwenye shughuli zao za uzalishaji mali na kulazimika kutembea umbali mrefu kutokana na vyombo vya usafiri kushindwa kufika katika maeneo waliyokuwa wanaelekea.
Walioathirika zaidi katika hili ni wale waliokuwa wakienda zaidi Kivukoni, eneo ambalo liko jirani na Ikulu na Makumbusho ya Taifa na Mikocheni ambako Kamala alitembelea.
“Haya ni mateso, yaani tunatembea umbali wote huu labda huko hata mazungumzo hawajamaliza. Hawa wanazuia magari watatufanya tuwachukie wageni. Kuna maana gani kama wageni wakija shughuli zetu zisimame,” alisikika mwanamke mmoja akilalama huku akitembea.
Kufungwa kwa barabara hizo kulisababisha msongamano wa magari kuongezeka kwenye barabara nyingine, huku kilio kikubwa kikiwa kwa madereva na makondakta wa daladala.
Kondakta wa daladala linalofanya safari zake Kisewe–Kivukoni alisema kutokana na foleni kubwa, walitumia takribani saa tatu kutoka Kisewe hadi mjini ambako hata hivyo hawakufanikiwa kufika hadi Kivukoni.
Ulinzi usipime
Wakati barabara zikiwa hivyo, hali ya ulinzi ilionekana kuimarishwa katika maeneo yote ambayo Kamala alipita na kutembelea, ikiwemo Makumbusho ya Taifa.
Lango kuu la Makumbusho lilizungukwa na watu wa usalama wa Tanzania na Marekani, wakiruhusiwa watu maalumu kuingia, wakiwemo waandishi wa habari wenye kadi maalumu.
Ukaguzi wa hali ya juu uliohusisha teknolojia ya kisasa ulikuwa ukifanyika kwa wote walioingia eneo hilo, kazi hii ilifanyika saa moja na nusu kabla ya Kamala kuwasili.
Jana wakati akiondoka, hali ilikuwa hivyo pia kwa barabara kadhaa kufungwa kwa muda kupisha msafara wake kwenda uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) ambako aliagwa rasmi na Makamu wa Rais, Dk Phillip Mpango na ndege yake kupaa saa 5:35 asubuhi.
Awakutanisha viongozi
Katika futari aliyoandaliwa Harris na Rais Samia, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, wa Serikali na wastaafu walijumuika pamoja, jambo ambalo halijawahi kutokea miaka ya hivi karibuni.
Miongoni mwa wanasiasa wa upinzani waliohudhuria dhifa hiyo ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe.
Pia, alikuwepo Makamu Mwenyekiti wa CCM, Abdulrahman Kinana na Rais mstaafu, Jakaya Kikwete.
Katika ukurasa wake wa kijamii wa Twitter, Mbowe ameweka picha hiyo na kuandika “Jana (juzi) nilipata wasaa wa kukutana na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na viongozi wengine kwenye iftar iliyoandaliwa kwa ajili ya Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, ikulu, Dar es Salaam.”
Rais Samia amshukuru
Rais Samiaaliandika katika ukurasa wake wa Twitter akimshukuru Harris kwa kutembelea Tanzania na kwamba, safari hiyo itasukuma utekelezaji wa mambo waliyojadiliana na kuimarisha uhusiano baina yao.
“Asante Mheshimiwa Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris kwa safari yako ya kihistoria Tanzania. Safari hii na utekelezaji wa tuliyojadiliana vitasukuma uhusiano wa Tanzania na Marekani kwenda mbele zaidi kwa manufaa ya nchi zote mbili. Safari njema na karibu tena Tanzania,” aliandika Rais Samia.
Manufaa ya ziara
Ziara ya kiongozi huyo hapa nchini imekuwa na mafanikio kwa sababu Marekani itatoa Dola 400,000 (Sh935.7 milioni) kusaidia Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), ili kuwaleta pamoja wadau kujadili zaidi mageuzi ya kidemokrasia na kisheria, wakati huo huo kikijenga uwezo wa vijana kushiriki katika siasa.
Lengo la msaada huo ni kusaidia azma ya Tanzania ya kuimarisha demokrasia, hususan nchi inapoelekea kwenye chaguzi za mwaka 2024 na 2025.
Juzi, Shirika la Marekani la Ushirikiano wa Kimataifa (USAID) na Tanzania zilisaini makubaliano ya miaka mitano ya msaada wenye thamani ya Dola za Marekani 1.1 bilioni (Sh2.5 trilioni). Katika makubaliano hayo, USAID itafanya kazi kwa karibu na Serikali ya Tanzania kutoa msaada katika maeneo ya ukuaji uchumi, afya, elimu, demokrasia na utawala bora.