Sababu mgomo wa daladala Dodoma uliodumu kwa saa tano hii hapa

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Ubovu wa miundombinu ya kituo cha daladala cha Sabasaba jijini Dodoma imetajwa kuwa chanzo cha mgomo wa madereva uliodumu kwa saa tano leo Jumatano Januari 13, 2021.

Dodoma. Ubovu wa miundombinu ya kituo cha daladala cha Sabasaba jijini Dodoma imetajwa kuwa chanzo cha mgomo wa madereva uliodumu kwa saa tano leo Jumatano Januari 13, 2021.

Madereva hao walifanya mgomo huo kushinikiza kuboreshwa kwa mazingira ya eneo hilo yanayoharibika kila msimu wa mvua.

Mgomo huo ulisababisha abiria wanaokwenda maeneo mbalimbali wakiwemo wanafunzi kukosa usafiri na wengine kulazimika kutumia bajaji na bodaboda.

Mmoja wa madereva hao, Hashim Salum amesema ubovu wa miundombinu katika kituo hicho umesababisha magari yao kuharibika mara kwa mara.

 “Yaani hapa huwezi kwenda tripu mbili kabla ya kurudi gereji, vyuma vinakatika kutokana na mabonde yenye mawe yaliyopo katika kituo hiki,” amesema Salum.

Amesema kituo hicho kina changamoto nyingi ikiwemo ubovu wa miundo mbinu, hakuna taa za barabarani na wafanya biashara wadogo kuwa wengi ndani ya kituo jambo ambalo linasababisha kuwepo kwa hatari ya kutokea kwa ajali.

“Kwa ufupi tu ni kwamba, hapa hakuna mpangilio kama kwenye vituo vingine vya daladala. Mfano mzuri ni Morogoro au Tabora. Kwa nini tusitengewe eneo maalum? alihoji Hashim

Dereva mwingine Patrick Joseph amesema waliamua kugoma kwa sababu uongozi umekuwa ukipuuza malalamiko yao kwa muda mrefu.

Amesema lengo la mgomo huo ni kufikisha ujumbe kwa mamlaka husika maana walilalamika kwa muda mrefu bila suluhu .

Akizungumza na madereva hao mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Josephat Maganga aliwasihi kuendelea na shughuli zao za kila siku.

Maganga aliwataka pia wachuuzi wote waliopo ndani ya au katika eneo la kituo cha daladala kuhama kwa sababu kuendelea kukaa katika eneo hilo wanahatarisha maisha.

Mgomo huo ulimalizika baada ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuhamishia daladala hizo katika eneo la Bohari ili kutoa nafasi ya kutengezwa kwa kituo hicho cha Sabasaba.

Alipoulizwa kuhusu hatua zilizochukuliwa ili kuboresha kituo hicho Sabasaba, mhandisi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ludigija Ludigija amesema jambo linalofanyika hivi sasa ni kuziba mashimo yaliyoko kwenye kituo hicho cha Sabasaba.

“Tumeshapanga pia kuzigawanya daladala katika kituo kipya cha Makole B Center ambacho kitakuwa na uwezo wa kuchukua daladala kati ya 100 hadi 150,”amesema.

Amebainisha kuwa chanzo cha kuharibika mara kwa mara na msongamano katika kituo cha Sabasaba ni wingi wa daladala na ndio maana wameamua kuzipunguzia katika kituo hicho kipya.

Amesema hali hiyo itakifanya kituo cha Sabasaba kubakia na daladala kati ya 200 hadi 250.

 “Vituo vyetu vingi vya daladala haviko katika hali nzuri sana. Vingi vipo katika hali ya changarawe. Lakini hivi sasa tunategemea kufanyia maboresho vituo vya Nzuguni, Kikuyu, Mnadani na Chang’ombe pia,” amesema.