Sababu ufaulu kuongezeka Zanzibar yatajwa

Sababu ufaulu kuongezeka Zanzibar yatajwa

Muktasari:

  • Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili, darasa la sita na la nne mwaka 2020 yakionyesha kuwa ufaulu umepanda.

Unguja. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha pili, darasa la sita na la nne mwaka 2020 yakionyesha kuwa ufaulu umepanda.

Akizungumza leo Jumanne Januari 26, 2021 waziri wa elimu, Simai Mohammed Said  amesema kupanda kwa ufaulu kunatokana na ushirikiano mzuri kati ya walimu, wazazi na wizara hiyo.

Amesema watahiniwa 25,593 sawa na asilimia 78.67 waliofanya mtihani wa kidato cha pili kati ya 32,279 waliofanya mtihani huo wamefaulu na waliofeli ni 6,886 sawa na asilimia 21.33.

Amesema wilaya zote zimefanya vizuri huku wilaya ya Chakechake ikiongoza kwa ufaulu wa asilimia 86.89 na wilaya ya Kusini ni ya mwisho yenye iliyopata asilimia  61.32.

Kuhusu matokeo ya darasa la nne amesema watahiniwa 39,273 sawa na asilimia 81.4 wamefaulu.

Amebainisha kuwa kati yao, wasichana ni 21,162 sawa na asilimia 43.86 na wanaume 18,111 sawa na asilimia 37.54. amesema wanafunzi  8,973 sawa na asilimia 18.6 ya wanafunzi wote hawakufaulu.

“Katika mtihani wa darasa la nne wilaya ya mjini inaongoza kwa ufaulu wa jumla kwa kuwa na asilimia 91.26 ikifuatiwa na Wilaya Chake Chake yenye asilimia 87.35. Wilaya ya Mkoani ni ya mwisho kwa kuwa asilimia 67.42 ya ufaulu,” amesema.

Said  amesema katika mtihani wa darasa la ufaulu unaonesha kuwa  watahiniwa 32,462 sawa na asilimia 98.34 kati ya 33,010 waliofanya mtihani huu wamefaulu na waliofeli ni watahiniwa 548 sawa na asilimia 1.66.

Amesema wilaya zote zimefanya vizuri zikiongozwa na wilaya ya Micheweni iliyopata asilimia 99.78 ikifuatiwa na Wilaya Chake Chake iliyopata asilimia  99.05.