Sababu za Jaji Siyani kujitoa kusikiliza kesi ya Mbowe na wezanke

Muktasari:

  • Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu.

  

Dar es Salaam. Jaji Kiongozi, Mustapha Siyani amejitoa kusikiliza kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe na wenzake watatu.

Siyani ameeleza leo Jumatano Oktoba 20, 2021 sababu ya kujitoa kusikiliza kesi hiyo ni kutokana na majukumu aliyoyanayo ambayo ameona yanaweza kumfanya ashindwe kuendesha kesi kwa haraka.

" Ninavyoona kesi hii inahitaji kusikilizwa kwa haraka na nikiangakia inaweza kuchukua miezi miwili ya usikilizwaji, hivyo kutokana na majukumu ya ziada niliyopewa, sitaweza kuendelea kusikiliza kesi hii, hivyo naamua kujitoa kusikiliza kesi hii" Amesema Jaji Siyani ambaye ameteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwa Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu Oktoba 8, 2021.

" Hivyo mtapewa jina la jaji ambaye ataendele na shauri hili na tarehe ya kusikiliza kesi hii ambayo inatakiwa kwenda kwa haraka kutoka kwa Msajili wa Mahakama, kwa sababu hiyo napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru sana kwa ushirikiano wenu" Amesema Jaji Siyani na kisha kunyayuka katika kiti chake alichokuwa amekaa ndani.

Mbowe na mwenzake, wanakabiliwa na mashtaka sita likiwemo la kula njama na kutoa fedha kwa ajili ya kutenda vitendo vya kigaidi katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

Hii ni mara ya pili kwa kwa jaji anayesikiliza kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 16/2021, kujioandoa kusikiliza shauri hilo.

Kwa mara ya kwanza, Septemba 6, 2021, Jaji Elinaza Luvanda alijiondoa kusikiliza shauri hiyo, baada ya washtakiwa wote katika kesi hiyo kumkataa.

Washtakiwa hao walimkataa Jaji huyo kwa madai kuwa hawana imani na Jaji Luvanda katika kutenda haki dhidi ya kesi yao.

Kabla ya kujiondoa katika kesi hiyo, Jaji Siyani ametoa uamuzi katika kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi, ambapo ametupilia mbali mapingamizi mawili yaliyokuwa yamewekwa na upande wa utetezi na kupokea maelezo onyo ya mshtakiwa Adam Kasekwa ambayo kwa sasa yatatumika katika kesi hiyo.

Kwa maana hiyo, kesi hiyo imeahirishwa hadi hapo Mahakama hiyo itakapopangiwa Jaji mwingine na washtakiwa wataendelea kubaki rumande.


Mbali na Mbowe , washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Hassan, Adam Kasekwa na Mohamed Ling'wenya.