Sababu zinazowakwamisha wanawake kuwa wanasheria zatajwa, wapewa moyo

Muktasari:

Wanawake kukosa ujasiri wanapokabiliwa na changamoto ni sababu iliyotajwa na baadhi ya wanasheria nchini Tanzania kuwa inachangia idadi ndogo ya wanawake wanasheria ikilinganishwa na wanaume.

Dar es Salaam. Wanawake kukosa ujasiri wanapokabiliwa na changamoto ni sababu iliyotajwa na baadhi ya wanasheria nchini Tanzania kuwa inachangia idadi ndogo ya wanawake wanasheria ikilinganishwa na wanaume.

Wakizungumza jana Machi 6, 2021  katika mkutano wa mawakili ulioandaliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) iliofanyika kwa njia ya mtandao wa Zoom, wanasheria hao wamesema wanawake wana nafasi kubwa ya kuitetea jamii katika kesi za maslahi ya umma.

Akitoa mada katika mkutano huo mhadhiri wa sheria kutoka Shule ya Sheria ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Natunjwa Mvungi amesema licha ya wanawake wengi kujiandikisha shule ya sheria ili kuwa mawakili wanaomaliza na kuendelea na kazi hiyo ni wachache.

“Mwaka 2017 wanawake waliosajiliwa walikuwa  206 na wanaume 317, mwaka 2018 kulikuwa na wanaume 315 na wanawake 320, mwaka 2019 wanaume 334 wanaume  317 na mwaka 2020 walikuwa mawakili wanaume 279 na mawakili wanawake 255.”

“Utaona wakati wa kujiandikisha kunakuwa na wanawake wengi, lakini ukiendelea mbele wengi hawaendelei. Swali la kujiuliza kwa nini hawaendelei,” amehoji.

Dk Mvungi alimtaja aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Fatma Karume na kubainisha kuwa sababu  zinazowakwaza wanawake katika shughuli za uwakili ni vitisho na kuonekana maadui wa jamii.

“Utaona watu wanaozungumza sana kwenye jamii wanapata vitisho na maneno makali. Baadaye unaonekana adui na wengine wanasema hiyo ni kazi ya wanaume,” amesema.

Naye Flaviana Charles ambaye ni mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu (WHRDs) amesema mbali na vitisho wanavyopata, wanawake pia wanakabiliwa na ukosefu wa fedha, vikwazo, kubanwa na mambo ya familia, matatizo ya lugha mahakamani.

“Kinachotakiwa ni kujiunga na mawakili wazoefu, kutafuta wakufunzi wazoefu, kutafuta uzoefu wa wanasheria wa kimataifa, tafuta maarifa zaidi, uwe tayari kujifunza na hakikisha unakwenda na wakati na teknolojia,” amesema. 

Akitoa mada katika mkutano huo, Rais mstaafu wa TLS  John Seka amesema licha ya uchache wa wanawake katika fani ya sheria, idadi yao imekuwa ikiongezeka kwa kasi miaka ya hivi karibuni.

Huku akirejea hukumu za Jaji mstaafu James Mwalusanya, amesema katika moja ya hukumu zake, Jaji huyo aliwahi kusema ‘Kuanzia sasa wanawake Tanzania wanaweza kuinua vichwa vyao na kuongoza njia.’ Je, alichokisema Jaji Mwalusanya kuhusu wanawake katika uongozi na jinsi ya kufikia usawa wa kijinsia kimefikiwa?”

Amesema licha ya ongezeko hilo la wanasheria wanawake, matatizo ya wanawake katika jamii nayo yameongezeka.


“Wanawake wengi bado wanalalamikia unyanyasaji wa kijinsia ofisini na shule, wengine wanalalamikia kutokuwepo kwa malipo sawa kati yao na wanaume, bado kuna changamoto ya wanawake kumiliki mali, wasichana wanafukuzwa shule wakipata mimba.”

“Ninaleta haya matatizo kwa sababu nataka kuonyesha alichomaanisha Jaji Mwalusanya ili niwape hasira,” amesisitiza.

Awali akifungua mkutano huo, Jaji Dk Lilian Mongella amesema idadi ya mawakili wanawake inazidi kuongezeka na kwa sasa wapo zaidi ya 3,000 waliosajiliwa TLS kati ya zaidi ya mawakili 7,000.