VIDEO: Sabaya kortini peke yake leo

Sabaya kortini peke yake leo

Muktasari:

Sabaya ametinga kortini peke yake baada ya wenzake wanne aliokuwa akishitakiwa nao kuachiliwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi Septemba 6, baada ya kukiri makosa na kuhukumiwa na kulipa faini.

Moshi. Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amefikishwa mahakamani leo kwa mara ya kwanza bila kuwa na wenzake wanne ambao Septemba 6 waliachiliwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi.

Sylvester Nyegu, John Aweyo, Nathan Msuya na Antero Assey ambao walikuwa ni washirika wa Sabaya walitiwa hatiani baada ya kukiri kutenda makosa ya uhujumu uchumi.

Baada ya kutiwa hatiani, washitakiwa hao kila mmoja alihukumiwa kulipa faini ya Sh50,000 na Sh1 milioni kama fidia kwa mwathiriwa na baada ya kutimiza vigezo hivyo waliachiliwa huru.

Makosa waliyokutwa nayo ni makosa mawili, moja kujitwalia madaraka isivyo halali na kwenda kufanya upekuzi nyumbani kwa Alex Swai na kosa la pili kula njama na kumnyima na kukandamiza haki ya mhanga ambaye ni Alex Swai kwa madai ya kukwepa kulipa kodi.

Sabaya na wenzake wanne walifikishwa katika mahakama hiyo Juni Mosi mwaka huu wakikabiliwa na tuhuma mbalimbali ikiwemo uhujumu uchumi.