Samia asisitiza ulipaji kodi, kufanya kazi kwa bidii

Samia asisitiza wananchi kulipa kodi, kujiepusha na rushwa

Muktasari:

  • Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amewasihi watumishi wa Serikali na sekta binafsi kufanya kazi na kupata kipato halali huku wakijiepusha na wizi, rushwa na ubadhilifu.

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania,  Samia Suluhu Hassan amewasihi watumishi wa Serikali na sekta binafsi kufanya kazi na kupata kipato halali huku wakijiepusha na wizi, rushwa na ubadhilifu.

Pia, amewaomba wafanyabiashara kulipa kodi na kuacha kuikwepa kwa maelezo kuwa kufanya hivyo kutaifanya  Serikali ishindwe kutoa huduma kwa wananchi.

Ameeleza hayo  leo jioni Ijumaa Mei 14, 2021 katika baraza la Idd lililofanyika katika viwanja vya Karimjee mkoani Dar es Salaam.

“Nawaomba tuendeleze ucha Mungu tuliouonyesha kwa kipindi cha mwezi  mtukufu wa Ramadhani, usiishie jana baada ya mwezi kuandama.”

“Natumia fursa hii kuwasihi watumishi wote wa Serikali na sekta binafsi kufanya kazi halali wajiepushe na vitendo vya wizi, rushwa ubadhilifu na urasimu na wafanyabiashara lipeni kodi stahiki kwa Serikali ili iweze kutoa huduma kwa wananchi,” amesema.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema wafanyabiashara kutolipa kodi watasababisha hospitali  kukosa dawa na kusababisha vifo, watumishi watakosa mishahara na haki zao stahiki na wanafunzi watakosa elimu bure.

“Ninawaomba kuendelea kuishi na matendo mema kama tuliyoonesha kwa kipindi chote cha mfungo, tukifanya hivyo baraka zote tulizozipata,  zitaendelea kuishi nasi pia napongeza umoja ulioonyeshwa  bila kujali tofauti za dini,” amesema Samia.