Samia: Kodi za dhuluma hapana

Tuesday April 06 2021
kodipic

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitaka Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuangalia namna bora ya kuwarudisha wafanyabiashara waliofunga biashara zao kutokana na mabavu yalikuwa yakitumika kwenye ukusanyaji kodi.

Amesema ukusanyaji wa kodi kwa kutumia nguvu na mabavu hausaidii umesababisha wafanyabiashara wengi kufunga biashara zao kwa kuhofia kubambikiwa kesi.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ameeleza hayo leo Jumanne Aprili 6, 2021 baada ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao Ikulu jijini Dar es Salaam na kumtaka bosi wa TRA, Alphayo Kidata kuhakikisha taasisi hiyo inakusanya kodi kwa haki bila kuwaumiza wafanyabiashara.

“Kukusanya kodi kwa mabavu havisaidii kwa muda mrefu. Nimepewa takwimu ya zile taskforce mlizoziunda lakini haisaidii, mnawatisha watu wanalazimika kufunga biashara.”

“Tunazitaka lakini kodi za dhuluma hapana. Kwa sababu hazitatufikisha mbali. Jinsi ya kurudisha wafanyabiashara, kutengeneza wigo wa kukusanya biashara, nafahamu uamuzi huu niliochukua tutayumba kwa miezi miwili mitatu lakini  baada ya muda tutarudi vizuri,” amesema Samia.

Advertisement