Samia kumalizia viporo vya watangulizi wake?

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa na wajumbe wa kamati ya marishiano kutoka Chadema na CCM. Picha na Maktaba

Muktasari:

  • Julai Mosi, mwaka huu tumeadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Ni muda mrefu. Kama ni maisha ya binadamu huu ni umri wa mtu mzima, ambaye pengine tayari ana familia na anajitegemea kikamilifu.


Na Kitila Mkumbo

Julai Mosi, mwaka huu tumeadhimisha miaka 30 tangu kuanzishwa tena kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Ni muda mrefu. Kama ni maisha ya binadamu huu ni umri wa mtu mzima, ambaye pengine tayari ana familia na anajitegemea kikamilifu.

Ni muda mzuri wa kuangalia nyuma na kupima mafanikio yaliyopatikana katika demokrasia yetu na mchango wake katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni.

Hatua ya kwanza ya kupima mafanikio ya kitu au jambo lolote ni kuona kama jambo au kitu hicho kimefanikiwa kuendelea kuwepo. Hata katika vita muhimu kuliko vyote ni kuhakikisha kwamba jeshi halipotezi askari. Uwepo ndio kipimo cha kwanza cha mafanikio.

Vyama 10 vilipata usajili wa kudumu kati ya Julai 1, 1992 na Novemba 24, 1993. Chama cha kwanza kabisa kupata usajili wa kudumu kilikuwa ni CCM, kilichopata usajili wake Julai 1, 1992. Vyama vingine vitano vilifuata miezi sita baadaye, vikipata usajili wao Januari 21, 1993. Vyama hivi ni CUF, Chadema, UMD, NCCR-Mageuzi na NLD.

Hadi uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi unafanyika mwaka 1995 tulikuwa na vyama vyenye usajili wa kudumu 11. Kwa mujibu wa taarifa zilizopo katika tovuti ya Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, hadi sasa tuna vyama vya siasa 19 vyenye usajili wa kudumu.

Chama cha hivi karibuni kabisa kusajiliwa ni ACT-Wazalendo, kilichosajiliwa Mei 5, 2014. Kwa hivyo, kwa kigezo cha uwepo, tunaweza kusema kwamba mfumo wa vyama vingi umefanikiwa kubaki na uhai wake kwa kipindi chote cha miaka 30, ukiacha vyama vichache vilivyofutwa kama vile chama cha TPP.

Eneo la pili katika kutathimini mafanikio ya miaka 30 ya mfumo wa vyama vingi nchini ni kiwango cha ushindani wa vyama vya siasa. Kawaida, mafanikio ya kisiasa hatimaye hupimwa kwa kuangalia namba. Siasa ni hesabu.

Umuhimu wa chama katika mchakato wa kisiasa katika nchi yoyote hatimaye hupimwa kwa kuangalia kiwango ambacho chama hicho kinashiriki katika kufanya maamuzi kupitia vyombo vya maamuzi. Vyombo hivi ni Serikali, Bunge na Madiwani.

Kwa kuzingatia kigezo hiki, ni wazi kwamba mafanikio ya mfumo wa vyama vingi katika eneo hili ni madogo sana.

Hii ni kwa sababu katika chaguzi zote chama kimoja, CCM, kiliendelea kupata ushindi katika ngazi zote za uchaguzi kwa kiwango ambacho kilipata uhalali wa kufanya maamuzi bila kutegemea ushiriki wa vyama vingi.

Kwa mfano, ukiacha ukweli kwamba CCM ilifanikiwa kushinda nafasi ya urais katika chaguzi zote, katika nafasi ya ubunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tangu kuanza kwa uchaguzi wa mfumo wa vyama vingi CCM haijawahi kupata chini ya theluthi mbili ya viti vya ubunge.

Ni katika chaguzi mbili tu (kati ya sita) ambapo CCM ilipata chini ya asilimia 80. Chaguzi hizi ni za mwaka 2010 ambapo CCM ilipata asilimia 79.1 ya viti bungeni na mwaka 2015 ambapo CCM ilipata asilimia 73.6 ya viti Bungeni. Katika chaguzi nyingine CCM ilipata asilimia zifuatazo za wabunge: 1995 (80.2%), 2000 (87.1%), 2005 (88.8%), 2020 (95.6%).

Kwa hiyo, katika miaka yote 30 ya mfumo wa vyama vingi ni chama kimoja tu (CCM) ambacho kimekuwa na uwezo wote wa kufanya maamuzi katika chombo muhimu cha kutunga sheria, yaani Bunge. Ndiyo kusema, kwa kuzingatia kigezo hiki, tunaweza kusema bila shaka kuwa mfumo wetu wa vyama vingi haukui, bali umedumaa!

Aidha, kwa kuzingatia kigezo hiki, katika kipindi hiki CCM imeendelea kushamiri kisiasa. Hii inaweza kutafsiriwa kuwa CCM imeendelea kutoa sera na uongozi bora zaidi ukilinganisha na vyama vingine na pengine ndiyo sababu ya msingi kwa nini wananchi waliendelea kuichagua kwa wingi wa kura kiasi hicho.

Eneo la tatu katika kutathimini maendeleo ya mfumo wa vyama vingi nchini ni kuangalia kiwango cha ukuaji wa demokrasia. Neno demokrasia lina tafsiri nyingi. Tafsiri ya msingi kabisa kuhusu demokrasia ni kuiangalia dhana ya demokrasia katika muktadha wa kuiona kama nyenzo ya kulinda uhuru.

Uhuru ni bidhaa muhimu sana kwa binadamu na moja ya vigezo vya kututofautisha sisi binadamu na wanyama wengine. Zipo aina tatu kuu za uhuru. Kwanza, ni uhuru wa nchi; yaani uwezo wa wananchi na nchi yenyewe kujipangia maisha yao, wakijitawala wenyewe bila kuingiliwa na nchi nyingine au mtu mwingine.

Huu ndio uhuru tuliopigania kutoka kwa wakoloni. Uhuru wa pili ni uhuru wa kutosumbuliwa na njaa, maradhi na ujinga. Ni uhuru unaopatikana kwa njia ya kujikomboa kiuchumi. Uhuru wa tatu ni uhuru wa kukusanyika, kutoa maoni, kushiriki katika kutoa maamuzi yanayohusu maisha yake kwa kuzingatia sheria zilizopo.

Sambamba na uhuru, demokrasia pia hupimwa kwa kuangalia kiwango cha utawala wa sheria katika nchi husika na jinsi ambavyo kila mtu anawajibika kutii sheria bila kuangalia hali yake.

Aidha, kigezo kingine cha kupima maendeleo ya demokrasia ni kuangalia kiwango cha kukua kwa utamaduni wa kidemokrasia. Utamaduni wa kidemokrasia hudhihirika pale ambapo jamii inajenga utamaduni wa kutofautiana kimawazo na kimtazamo bila kudharauliana au kugombana. Utamaduni huu ndio hatimaye huweka sera kudhaa na mikakati mbadala katika kujibu changamoto za jamii husika.

Ni wazi kuwa bado kuna changamoto nyingi katika kufikia kiwango cha kuridhisha cha ujenzi wa demokrasia. Hii inadhihirishwa na mambo mawili makubwa.

Mosi, ni ukweli kwamba utamaduni wa kidemokrasia bado haujajengeka kwa kuzingatia kuwa uhuru wa kutoa maoni bila hofu wala woga haujashamiri kutokana na vikwazo vya kisheria na vya kiutamaduni.

Jamii yetu imejengwa katika msingi wa nenda na walio wengi na kuheshimu yote yasemwayo na wakubwa kama vile wazazi, walimu na viongozi. Utamaduni huu umejenga woga na hofu ya kwenda kinyume na mawazo ya watu wengine, hasa viongozi.

Pili, yamekuwepo malalamiko ya vyama vya upinzani kwa miaka mingi juu ya kukosekana kwa usawa katika uwanja wa siasa baina ya chama tawala na vyama vya upinzani.

Vyama vya upinzani vinaamini kwamba vimekuwa vikionewa na vyombo vya dola, hasa ukizingatia kwamba wakuu wa vyombo hivi vyote huteuliwa na Rais ambaye katika chaguzi mbalimbali za urais amekuwa ni mgombea mmojawapo.

Ni katika muktadha huu tunalazimika kuitupia jicho la pekee makala ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, aliyoandika Julai 1, 2022 na kuchapishwa katika magazeti mbalimbali, likiwemo la Mwananchi.

Katika makala hii Rais Samia alieleza falsafa yake ya uongozi inayobebwa na 4R (Reconciliation, Resilience, Reform and Rebuilding). Katika muktadha wa makala hii R ya Reform (mabadiliko) ina umuhimu wa pekee. Rais ameeleza kwa uwazi kuhusu dhamira yake ya kufanya mabadiliko katika mifumo ya kisiasa, kiuchumi na katika sheria za uchaguzi.

Aidha, Rais ameeleza kwa uwazi kuwa lengo lake ni kuona kuwa kunakuwa na ushindani wa haki na kuwapa wananchi fursa ya kuwachagua watu wanaotaka kuwaongoza.

Ni wazi kuwa kwa kuweka mkazo katika kuleta mageuzi katika mfumo wa kisiasa, kiuchumi na sheria za uchaguzi Rais anakubaliana na uwepo wa katiba mpya.

Hii haijidhihirishi katika makala yake tu, lakini pia katika ukweli kuwa yeye ndiye aliyepata heshima ya kuwa Makamu Mwenyekiti wa Bunge la Katiba. Itakumbukwa kuwa suala la Katiba mpya limekuwepo tangu wakati wa mjadala wa mfumo wa vyama vingi. Suala la uwepo wa Katiba mpya lilipendekezwa kwa mara ya kwanza na Tume ya Jaji Francis Nyalali iliyokusanya maoni kuhusu mfumo wa siasa unaofaa nchini.

Aidha, Tume ya Nyalali ilipendekeza kufumuliwa kwa mfumo wa sheria za uchaguzi ili kuvipa vyama vyote fursa sawa katika kufanya shughuli za siasa. Haya ni mapendekezo ambayo hayakutekelezwa kikamilifu katika awamu zote za uongozi wa nchi yetu.

Rais Mwinyi alitekeleza pendekezo moja kubwa la kukubali kuanzishwa tena kwa mfumo wa vya vingi, lakini akaliweka kiporo suala la kuandika Katiba mpya.

Suala hili lilikuja kupata nafasi mwaka 2011, pale Rais Kikwete alipoamua na hatimaye kukishawishi Chama cha Mapinduzi kukubali kuanzisha mchakato wa kuandika Katiba mpya. Hata hivyo, mchakato huu haukufika mwisho na umebaki kiporo hadi leo.

Makala ya Rais Samia inaleta matumaini kwamba katika kipindi chake cha uongozi kuna uwezekano mkubwa kwamba kiporo cha katiba mpya kitakamilishwa.

Aidha, ni wazi kuwa kuna uwezekano mkubwa malalamiko makubwa ya vyama vya upinzani kuhusu uwanja sawa wa siasa yakafanyiwa kazi katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Samia.

Tuendelee kumuombea Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili Mungu aendelee kumpa afya njema katika kutekeleza dhamira yake njema kwa nchi yetu.