Samia: Wizara ya Mawasiliano ishughulikie kupanda gharama za vifurushi

Tuesday April 06 2021
vifurushipic

Dereva akiendesha gari huku akisoma ujumbe kwenye simu yake kitu ambacho ni hatari kwa usalama wake kwani inaweza kusababisha kupa ajali. Picha na Said Khamis

By Peter Elias

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameitaka Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kushughulikia sakata la kupanda kwa gharama za vifurushi vya simu lililoibuka kuanzia Aprili 2, 2021.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi ameeleza hayo leo Jumanne Aprili 6, 2021 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya kuwaapisha makatibu wakuu na manaibu wao aliowateua Aprili 4, 2021.

 “Kulizuka rapsha rapsha juzi hapa kuhusu masuala ya mabando wananchi wakawa juu mkalituliza. Kalifanyieni kazi lisizuke namna ile, mpo na mnaangalia. Hawa watu wanakuja na mambo yao wananchi wanashtuka ndiyo na nyie mnashtuka, hapana,” amesema Rais Samia.

Amewataka watendaji wa wizara hiyo kukaa na wanaoendesha mitandao ya simu ili kupata ufumbuzi na kufanya kazi vizuri zaidi na kuitaka kujipanga zaidi kusambaza huduma ya mawasiliano katika maeneo yote nchini kwa sababu wafanyabiashara wanakwenda maeneo yenye biashara pekee.

“Kuna maeneo kuna Watanzania wetu wanataka mawasiliano lakini private sector haendi. Sisi kama serikali tunajipangaje kwenye mpango kazi wenu. Tutakapoita sekta tutataka nje na hayo,” amesema Rais Samia.

Ameitaka pia kuangalia ushindani wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) katika soko akibainisha kuwa bado haujawa mzuri, hivyo, waangalie cha kufanya ili lifanye vizuri.

Advertisement

Kuhusu mkongo wa Taifa, Rais Samia amesema kuna haja na kuwa na tamko la kisera kuhusu mkongo huo na sio wenye mitandao ya simu kuanzisha mikongo yao, jambo ambalo si salama kwa nchi.

Advertisement