SBL yawapika maofisa kilimo kwa vitendo

Muktasari:

  • Katika mpango kuimarisha kilimo nchini, Kampuni ya bia ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imetoa fursa ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa fani ya kilimo mkoani Kagera.

Bukoba.Katika mpango kuimarisha kilimo nchini, Kampuni ya bia ya Serengeti Breweries Limited (SBL) imetoa fursa ya mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa fani ya kilimo mkoani Kagera.

Mkurugenzi mtendaji wa SBL, Mark Ocitti amesema wanafunzi 17 wanaofadhiliwa na kampuni hiyo katika Chuo Kilimo Igabiro kilichopo mkoani Kagera wamepata fursa hiyo itakayosaidia kuimarisha kilimo nchini hivyo kutoa malighafi za kutosha viwandani.

“Tunayo programu ya kilimo viwanda inayowajengea wanafunzi uelewa kwa vimatendo ambao ni mfumo nje ya mafunzo yao ya kila siku darasani. Tun awapa nafasi ya kutembelea viwanda vyetu vya bia na mashamba ya wakulima tunaoshirikiana nao,” amesema Ocitti.

Kwa mwaka, SBL inanunua takriban tani 17,000 za nafaka sawa na asilimia 70 ya mahitaji yake ya uzalishaji kwa mwaka. Kuhakikisha kunakuwa na upatikanaji wa uhakika, kampuni hiyo inashirikiana na mtandao wa wakulima 400 kwenye mikoa minane nchini.

Licha ya wakulima, SBL inatoa ufadhili kwa wanafunzi wanaosomea fani ya kilimo hasa kutoka familia masikini hususan za wakulima wanaoshirikiana nao katika kilimo cha nafaka, malighafi wanazozitumia kwenye uzalishaji bia.

SBL inafanikisha haya yote kupitia program ya kilimo viwanda inayolenga kuwasaidia wanafunzi kutoka familia masikini kusomea diploma ya kilimo katika vyuo vya ndani. Ufadhili huo ulioanzishwa mwaka jana unahusu gharama zote za chuo na tayari wanafunzi 70 wamenufaika.

SBL inashirikiana na Kaole Wazazi College of Agriculture (Bagamoyo), Kilacha Agriculture Training Institute (Moshi) na Saint Maria Goretti Agriculture Training Institute cha Iringa kufanikish amafunzo hayo.

Mkuu wa Chuo cha Igabiro, Sadock Stephano amewaomba wadau wengine kuiga mfano wa SBL ili Taifa lipate wataalamu wa kutosha watakaosaidia kuinua mchango wa sekta ya kilimo kwenye kipato cha wananchi.