Sekta binafsi waenda Marekani kutangaza fursa Tanzania

Sekta binafsi waenda Marekani kutangaza fursa nchini

Muktasari:

  •  Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka sekta binafsi ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Angelina Ngalula,  umekwenda Marekani kwa ziara ya kibiashara ambayo imeandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na taasisi ya Corporate Council on Africa ya nchini Marekani.


Dar es Salaam. Ujumbe wa wafanyabiashara kutoka sekta binafsi ukiongozwa na Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi nchini (TPSF), Angelina Ngalula,  umekwenda Marekani kwa ziara ya kibiashara ambayo imeandaliwa na TPSF kwa kushirikiana na taasisi ya Corporate Council on Africa ya nchini Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Francis Nanai, wafanyabiashara hao waliondoka jana Septemba 16,  na wakiwa Marekani watakutana na wawekezaji wakubwa katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, utalii, miundombinu, kilimo na teknolojia ya habari.

Nanai ameeleza katika taarifa hiyo kwamba ziara hiyo ni sehemu ya jitihada za sekta binafsi za kuunga mkono juhudi za Serikali za kuboresha mazingira ya biashara na kuvutia wawekezaji wa nje na ndani pamoja na kuitangaza Tanzania.

“Ziara hii ni matokeo ya mkutano ambao mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi alifanya na Donald Wright, Balozi wa Marekani nchini Tanzania, ambapo Ngalula alimuomba kusaidia sekta binafsi ya Tanzania kwa kuwaunganisha na wawekezaji wakubwa wa Marekani,”

“Hii itawezesha kuwaunganisha wafanyabiashara wa Marekani na Tanzania katika utekelezaji wa miradi ya ubia na kuwekeza katika sekta za utalii, uvuvi, afya, miundombinu, ujenzi  na kukuza biashara na masoko kupitia mpango wa AGOA,” amesema Nanai.

Katika taarifa hiyo, Nanai ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani na Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kwa ushirikiano uliowezesha ziara hiyo.