Serikali kuanzisha ufugaji makao ya wazee

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Fatma Tawfiq akizungumza na wazee katika nakazi ya wazee wasiojiweza Njoro, Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Muktasari:

  • Kwa sasa yapo makao ya wazee 34, ambapo 14 ni ya serikali yenye wazee 261 na 20 yanaendeshwa na taasisi binafsi yakiwa na wazee 576.

Moshi. Serikali inakusudia kuanzisha ufugaji wa ng'ombe wa maziwa na kuku katika maeneo yenye makazi ya wazee wasiojiweza kwa lengo la kuboresha lishe kwa wazee na kupunguza gharama za uendeshaji.

 Hayo yamebainishwa leo Machi 18 na Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk John Jingu wakati akitoa taarifa ya makazi ya wazee wasiojiweza Njoro, kwa kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Ustawi na Maendeleo ya jamii.

Dk Jingu amesema kwa sasa yapo makao ya wazee 34, ambapo 14 ni ya serikali yenye wazee 261 na 20  yanaendeshwa na taasisi binafsi ambapo yana wazee 576 na kwamba setikali imeendelea na jitihada mbalimbali ili kuboresha majao hayo.

Amesema uanzishwaji wa miradi ya ufugaji, utasaidia kuongeza kipato katika makazi hayo ikiwa pia ni pamoja na kuwezesha wazee kufanya shughuli za uzalishaji.

"Zipo changamoto mbalimbali zinazokabili makazi haya ya wazee ikiwemo uhaba wa watumishi katika baadhi ya kada pamoja na kukosekana kwa usafiri wa gari.

“Serikali bado tuna mipango ya kuanzisha miradi ya ufugaji wa ng'ombe wa Maziwa na kuku, kwa ajili ya kuboresha lishe kwa wazee na kuongeza kipato ili kupunguza gharama za uzalishaji," amesema Dk Jingu.

Akizungumza katyika ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Fatma Tawfiq pamoja na mambo mengine amesema wataendelea kuishauri Serikali kuongeza bajeti katika kundi hilo ili kuboresha makazi ya wazee wasiojiweza ikiwa ni pamoja na kujenga mengine katika maeneo yenye uhitaji.

"Bado bajeti inahitajika ya kutosha ili kuboresha makazi ya wazee nchi nzima kwa sababu huu ni mfano, hivyo kamati kwa kushirikiana na wabunge wengine tutaendelea kuishauri serikali, ili iongeze bajeti," amesema.

Mwenyekiti huyo pia ameitaka jamii kuthamini na kuwajali wazee waliopo katika maeneo yao na kutambua kuwa uzee haukwepeki.