Serikali kuboresha huduma kwa watalii ili wakae siku nyingi nchini

DODOMA. Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imejipanga kuboresha huduma kwa watalii katika nyanja mbalimbali ili kuvutia watalii wengi zaidi ikiwa ni mkakati wa kuwafanya watalii hao kuongeza siku  za kukaa nchini na hatimaye kukuza pato la Taifa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja katika Kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kilichofanyika leo katika ukumbi wa Utawala Annex Bungeni jijini hapa.

Amesema moja ya mkakati wa Serikali ni kuboresha huduma za malazi kwa watalii kwa kuzirejesha hoteli za Wizara ambazo zinaendeshwa  na sekta binafsi ambazo kwa ujumla wake hazifanyi vizuri.

Amefafanua kuwa na Serikali inaendelea mikakati ya kuhakikisha hoteli hizo mara baada kurejeshwa  zinakuwa kinara kwa kutoa huduma bora kwa watalii.

Pia, amesema Serikali ina mkakati wa kuboresha maeneo ya fukwe na kuunganisha vifurushi vya safari za watalii.

“Tuna mpango wa kuomba umiliki wa maeneo ya fukwe urudi Serikalini ambapo moja ya mikakati yetu kama Serikali ni  kuunganisha vifurushi vya Watalii  ili waweze kutembelea vivutio vingi zaidi katika safari zao kwa mfano wakitoka hifadhini, waende kutembelea maeneo ya malikale na wamalizie safari zao katika maeneo ya fukwe, hii itawafanya watalii waweze kuongeza siku za kukaa nchini na kuongeza mapato ya utalii” amesema Masanja  

Katika hatua nyingine, Masanja amesema Serikali inaendelea kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na  kufanya utafiti wa kujua vivutio vipi vinapendwa zaidi.

“Moja ya mkakati wa Serikali ni kufanya utafiti wa vitu ambavyo watalii wanavipenda na pia kuvitangaza vivutio vya utalii na tumejifunza kwamba watalii wengi wanapenda kupumzika katika maeneo ya fukwe baada ya kutembelea maeneo ya hifadhi , malikale na mengineyo” amesema Masanja

Kuhusu ukarabati wa barabara kwenye maeneo ya hifadhi Masanja amesema Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege hifadhini pamoja na kuweka mazingira wezeshi ili watalii wanapofika wafurahie huduma.

Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Timotheo Mnzava ameishauri Serikali kuangalia namna bora ya kurahisisha mchakato wa uwekezaji wa mahoteli kwenye maeneo ya hifadhi ili kuboresha huduma za malazi kwa watalii.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Watendaji na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii na Taasisi zake.