Serikali kujenga mtaa wa viwanda, kituo cha biashara Dar

Serikali kujenga mtaa wa viwanda, kituo cha biashara Dar

Muktasari:

  •  Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mtaa wa viwanda na Kituo cha Biashara cha Kimataifa Kurasini ili kuchagiza uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya matumizi ya ndani na kuuza nje ya nchi.


Dar es Salaam. Serikali imeanza utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa mtaa wa viwanda na Kituo cha Biashara cha Kimataifa Kurasini ili kuchagiza uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya matumizi ya ndani na kuuza nje ya nchi.

Mradi huo pia unaelezwa kama sehemu ya jitihada za kuhakikisha Tanzania inanufaika na uanzishwaji wa Soko la Pamoja la Afrika (AfCFTA).

Septemba 9, mwaka huu Bunge la Tanzania liliridhia mkataba wa uanzishwaji wa AfCFTA, hivyo kuingia kwenye soko la watu bilioni 1.2 na uchumi wa thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 3.4 trilioni ambalo lilianza rasmi Januari mosi mwaka huu na hadi sasa zaidi ya nchi 40 kati ya 55 zimeridhia.

Akizungumza jana baada ya kushuhudia utiaji saini wa mikataba ya kuanza utekelezaji wa mradi huo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Profesa Kitila Mkumbo alisema mpango na matamanio yake ni kuona biashara zikifanyika katika eneo hilo kuanzia Juni mwakani.

“Tunatarajia hapa utafanyika uzalishaji wa bidhaa kwa ajili ya matumizi ya ndani na kuuza nje,” alisema Profesa Mkumbo.

Alisema katika mradi huo kutakuwa na viwanda vya kuchakata na kuongezea thamani mazao ya kilimo, viwanda vya kutengeneza na kuunganisha bidhaa mbalimbali, hususan za kielektroniki, soko la kimataifa la mazao ya kibiashara, maghala ya kuhifadhi uasili na ubaridi na kituo cha pamoja cha kutoa huduma.

“Mradi huu unatekelezwa kwa ubia wa Serikali na sekta binafsi, sisi kazi yetu ni kuweka mazingira vizuri kama hapa, tunaandaa na kuweka miundombinu yote muhimu ili wawekezaji wakija hapa ni kuwekeza tu. Tayari tumewapata watano wenye nguvu, michakato mingine inaendelea,” alisema Profesa Mkumbo.

Walioshinda zabuni ni DP World ya Dubai, Elsewedy ya Misri, Agility ya Dubai, Galco ya Tanzania na Shanghai Lingang Group Co. Limited ya China na mchakato unaofuata sasa ni wawekezaji hao kuwasilisha andiko la mradi ili kumpata mwekezaji au wawekezaji watakaoshirikiana nao kutekeleza mradi huo.

Kitila alisema Serikali imetenga Sh30 bilioni kwa ajili uandaaji wa eneo hilo kwa kuliwekea miundombinu ya umeme, maji, barabara, kujenga ukuta kulizunguka eneo na kumlipa mhandisi mshauri.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa EPZA, John Mnali alisema kampuni iliyoshinda kazi ya uendelezaji wa eneo lenye ukubwa wa ekari 56 ni Suma JKT Constraction na mhandisi mshauri ni kampuni ya Bico ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Kuhusu idadi ya viwanda vitakavyojengwa katika eneo hilo, Mnali alisema ni mpaka mhandisi mshauri atakapokamilisha mpango wa kina wa uendelezaji (Master Plan), kazi ambayo inatarajiwa kukamilika miezi mitatu ijayo.