Serikali kupunguza ada ya matangazo katika mabango

Serikali kupunguza ada ya matangazo katika mabango

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imependekeza kupunguzwa ada za matangazo katika mabango yanayowaka kutoka Sh18,000 hadi Sh13,000.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imependekeza kupunguzwa ada za matangazo katika mabango yanayowaka kutoka Sh18,000 hadi Sh13,000.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 10, 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Amesema mabango yasiyowaka yatatozwa  Sh15,000 hadi Sh10,000 wakati matangazo ya ukutani yakitozwa Sh15,000 hadi Sh10,000.

Kwa matangazo ya kielektroniki yamepunguzwa kutoka Sh20,000 hadi Sh10,000 na matangazo kwenye magari kutoka Sh15,000 hadi Sh10,000 kwa watangazaji wanaotangaza bidhaa za watu wengine.

Matangazo mengine ya muda mfupi au promosheni kwa siku kutoka Sh55,000 hadi Sh50,000 na kila bango 100 ya promosheni ya kwanza au sehemu ya fungu la mabango 100 ya kwanza kutoka Sh100,000 hadi Sh50,000.

Amesema kushushwa kwa ada hizo kutapunguza gharama za kutangaza biashara nchini na hatimaye kukuza ushindani kwenye biashara.