Serikali kushirikiana na wadau usambazaji nishati jadidifu

Dar es Salaam. Wakati athari za mabadiliko ya tabianchi zikiendelea kujidhihirisha nchini wadau wa nishati jadidifu kuendelea kushirikiana na serikali kuhakikisha teknolojia ya nishati hiyo inafika maeneo yote nchini.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Chama cha Nishati Jadidifu Tanzania (Tarea), Mhandisi Prosper Magali wakati wa kufunga Maonesho ya Kitaifa ya Nishati Jadidifu (Renewable Energy).

Magali alisema zipo changamoto mbalimbali wanazokabiliana kulifikia hilo ikiwemo uwezweshwaji wa sekta binafsi ili kuweza kupeleka teknolojia hiyo katika maeneo mbalimbali.

Alisema Serikali ikatanua wigo na kushirikiana na sekta binafsi ambayo itaongeza nguvu kwa kuwekeza katika sekta ndogo ya nishati jadidifu.

“Kuna mipango inayoendelea ya kuvutia sekta binafsi kuwekeza kwenye nishati jadidifu, inaweza kuchangia kufikia huko, kuna miradi ya umemejua pamoja na upepo ambayo inatarajiwa kutekelezwa,” anasema Magali.

Aliongeza kuwa ueneaji wa nishati hiyo katika maeneo yote nchini itawezesha kufikia lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia katika miaka 10 ijayo.

"Tunataka kushirikiana na serikali kuhakikisha tunapunguza matumizi ya kuni na mkaa kwa kuhamasisha matumizi ya teknolojia ya nishati jadidifu"alisema.

Akizungumza katika maonyesho hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA),Joel Laurent akimuwakilisha mgeni rasmi ambaye ni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema nishati jadidifu ina mchango mkubwa katika ukuaji wa sekta mbalimbali ikiwemo Kilimo ambayo ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.

Alisema kilimo kinahitaji matumizi ya zana mbalimbali ambazo nyingine huendeshwa kwa kutumia nishati.

Alitolea mfano kilimo cha umwagiliaji ambacho shughuli zake huitaji kuwemo kwa mitambo ambayo itasaidia umwagiliaji kufanyika kwa urahisi na ndani ya muda mfupi.

Pia nishati hiyo anaweza kuitumia katika vyombo vya usafirishaji pale anapotaka kusafirisha mazao au zana za kilimo kutoka eneo moja hadi jingine.

Alisema ueneaji na ukuaji wa  teknolojia hiyo pia utamsaidia kwa kiasi kikubwa mkulima kwani utasaidia nishati hiyo kupatikana kwa gharama nafuu hivyo kumsaidia mkulima kupunguza gharama

Ameongeza kuwa wao kama serikali wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha teknolojia hiyo inakuwa na kuenea katika maeneo mbalimbali.

"Tutaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakisha teknolojoa hizo zinakuwa na kufika katika maeneo mengi nchini"