Serikali kuwasaka walioiba vyakula, mali ajali ya Korogwe
Gari aina ya Coaster iliyokuwa imebeba maiti ikisafirisha kwenda kuzika mkoani Kilimanjaro baada ya kupata ajali iliyoua watu 20 wilayani Korogwe, Tanga.
Muktasari:
- Serikali imetoa wito kwa jeshi la polisi mkoani Tanga kuanzisha msako kwa wananchi walioiba vyakula, mali katika ajali iliyoua watu 20 wilayani Korogwe.
Korogwe. Mkuu wa mkoa wa Tanga, Omary Mgumba ameliagiza jeshi la polisi mkoani humo kuwatafuta na kuwakamata wananchi ambao wamekwenda kuiba kwenye tukio la ajali juzi usiku.
Akizungumza wakati wa shughuli za kuaga miili ya marehemu katika Hospitali ya Magunga wilayani Korogwe leo Jumapili Februari 5, 2023 amesema waokoaji hao walioiba wakamatwe.
Amesema kuwa jambo hilo sio jema na linatakiwa kukemewa kwa watu kujitokeza kwenye ajali, kisha kuchukua vitu vya waathirika badala ya kuwasaidia majeruhi.
"Kwa waokoaji kwenda kuwaokoa majeruhi, kwa kutoa miili pia kwenda kuwaibia, jeshi la polisi lipo watafuteni kwa njia zozote zile waliofanya vitendo vya kiharamu tunawatia nguvuni na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria", amesema Mgumba.
Amesema watu hao ambao bado hawajafahamika wameiba vyakula pamoja na mali nyingine kwenye tukio, badala ya kutoa msaada ambapo wameiba mpaka vyakula vilivyotakiwa kwenda kutumika msibani.
Aidha mwakilishi wa Mamlaka ya Uthibiti Usafiri Ardhini (Latra) ambae ni meneja usalama mazingira, Geoffrey Silanda amesema wamefuatilia mwenendo wa dereva aliyesababisha ajali na wanaandaa ripoti yao.
Amesema wameunda kamati kufuatilia tukio hilo kujua chanzo hasa cha ajali na taarifa itakabidhiwa kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
Kamanda wa kikosi cha usalama barabarani, Ramadhani Ngazi kwa upande wake amesema kutokana na tukio hilo wanakwenda kuangalia mfumo wa utoaji leseni na vyuo vya udereva nchini kuona utendaji wao kazi.
"Tumeagizwa tufanya uchunguzi kuhusu mfumo mzima wa utoaji wa leseni kwa madereva na mfumo wa shule za uendeshaji na mafunzo ya udereva ukoje na lengo la kikosi cha usalama kufanya hivyo ni ili kuhakikisha usalama wa wananchi wetu," amesema Ngazi.
Aidha idadi ya watu waliofariki kwenye ajali hiyo wilayani Korogwe imefikia 20 baada ya majeruhi wengine wawili kufariki.
Wawili hao walifariki mmoja akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya rufaa Bombo mkoani Tanga na mwingine Muhimbili.
Kutokana na kuongezeka idadi hiyo jumla ya marehemu kwa sasa wanafikia 21 ukiongeza na marehemu aliyekuwa akisafirishwa.