Serikali kuzifutia tozo hospitali za taasisi za dini

Serikali ya Tanzania yaeleza mkakati kuchochea uchumi shindani

Muktasari:

  • Serikali ya Tanzania imefuta tozo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa hospitali zinazomilikiwa na taasisi za  dini kutokana na kuisaidia Serikali kufikisha huduma za afya maeneo yasiyofikika.

Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imefuta tozo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa hospitali zinazomilikiwa na taasisi za  dini kutokana na kuisaidia Serikali kufikisha huduma za afya maeneo yasiyofikika.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi Juni 10, 2021 na Waziri wa Fedha na Mipango,  Dk Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha bungeni mapendekezo ya Serikali kuhusu makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2021/22.

Akielezea sheria ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi sura 82, Dk Mwigulu amependekeza kufanya marekebisho kwenye sheria hiyo kwa kufuta tozo ya elimu na mafunzo ya ufundi stadi kwa hospitali zinazomilikiwa na taasisi za dini.

“Taasisi hizi zimekuwa zikiisaidia sana Serikali kufikisha huduma za afya hata kwenye maeneo ambayo Serikali haijaweza kupeleka huduma kutokana na ufinyu wa bajeti,” amesema.

Amesema taasisi hizo zimekuwa na ushirikiano na Serikali kwa makubaliano maalum kwa baadhi ya maeneo ya kutoa huduma za afya, “lengo la hatua hii ni kutoa unafuu wa utoaji huduma za afya kwa vituo vya afya.”