Serikali: Ugonjwa ulioibuka Lindi ni homa ya Mgunda

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu

Muktasari:

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema vipimo vya maabara vimeonyesha ugonjwa ulioibuka mkoani Lindi ni homa ya Mgunda (Leptospirosis).

Dar es Salaam. Upimaji wa sampuli za wagonjwa waliokuwa wakiugua ugonjwa usiojulikana katika Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi umethibitisha mlipuko huu kuwa wa ugonjwa wa homa ya Mgunda ‘Leptospirosis, Field Fever’.

Hayo yamejulikana ikiwa ni siku nne zimepita tangu Serikali ya Tanzania ikubali ombi la Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha kukinga na kudhibiti magonjwa (CDC) kutoka Serikali ya Marekani kuongeza nguvu kwenye timu ya wataalamu katika kubaini ugonjwa huo.


Akizungumza leo Jumatatu, Julai 18, 2022 Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ametoa taarifa hiyo baada ya kutembelea Wilaya ya Ruangwa katika Mkoa wa Lindi ambako kumezuka mlipuko huo.

Waziri Ummy amesema kuwa Homa ya Mgunda ni miongoni mwa magonjwa yanayoambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu na unasababishwa na Bakteria aina ya Leptospira interrogans.

“Ugonjwa huu umekuwepo katika maeneo ya kitropiki ambayo ni yenye hali ya joto katika mabara ya Amerika ya Kaskazini, Amerika ya Kusini, Afrika, Asia na Australia. Wanyama aina za panya, kindi, mbweha, kulungu, swala, na wanyamapori wengine wameripotiwa kupata maambukizi ya vimelea hivi na kuwa chanzo cha maambukizi kwa binadamu” amesema Waziri Ummy

Amesema kuwa Ugonjwa wa Homa ya Mgunda huambukizwa kutoka kwa wanyama kwenda kwa binadamu kupitia uchafuzi wa mazingira ikiwemo vyanzo vya maji kutoka katika mkojo wa wanyama wenye maambukizi.


Unaambukizwaje?


Waziri Ummy amesema mtu anaweza kupata ugonjwa huo kwa kugusa mkojo (au maji maji mengine ya mwili) kutoka kwa wanyama wenye maambukizi; kugusa maji, udongo, au chakula kilichochafuliwa na mkojo wa wanyama wenye maambukizi au kunywa maji yaliyochafuliwa na vimelea vya bakteria wa ugonjwa huo huku maambukizi ya ugonjwa huu kutoka kwa binadamu mmoja kwenda kwa mwingine hutokea kwa nadra.

Julai 12, akihutubia Mkutano wa 20 wa Shirikisho la Baraza la Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati (Amecea) Rais Samia Suluhu Hassan alisema kuna ugonjwa mpya umeingia katika mikoa ya Kusini ambapo baadhi ya watu wanatokwa damu puani na kuanguka.

Kufuatia ugonjwa huo watu watatu wamefariki dunia kati 13 waliougua mkoani Lindi ambapo moja ya dalili zake ni kuvuja damu puani.