Serikali ya Tanzania kukopa Sh7 trilioni

Thursday June 10 2021
kukopapic
By Tatu Mohamed

Dar es Salaam. Serikali imesema inatarajia kukopa Sh7.34 trilioni kutoka soko la ndani na nje kwa masharti ya kibiashara.

Kati ya kiasi hicho, Sh4.99 trilioni ni mikopo ya ndani ambayo inajumuisha Sh3.15 trilioni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za Serikali zinazoiva na Sh1.84 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Akiwasilisha bajeti ya serikali leo Alhamisi Juni 10, 2021 bungeni mjini Dodoma Waziri wa Fedha na Mipango,  Dk Mwigulu Nchemba amesema Sh2.35 trilioni zinatarajiwa kukopwa kutoka soko la nje kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Kwa mwaka 2021/22 Serikali inapanga kutumia Sh36.33 trilioni kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo Sh23 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh13.33 trilioni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.”

“Fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida zinajumuisha Sh10.66 trilioni kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali, Sh8.15 trilioni kwa ajili ya mishahara na Sh4.19 trilioni kwa ajili ya matumizi mengineyo,” amesema.

Amesema Serikali imetenga Sh200.0 bilioni kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi,  wazabuni na watoa huduma.

Advertisement


Leo asubuhi wakati akiwasilisha bungeni hali ya uchumi wa Taifa kwa mwaka wa fedha 2020 na mpango wa maendeleo ya Taifa kwa mwaka wa fedha 2021/22, Dk Mwigulu amesema hadi kufikia Aprili 2021 deni la Serikali lilikuwa limefikia wastani wa Sh60.9 trilioni.


Amebainisha kuwa kati ya hizo,  deni la nje lilikuwa Sh43.7 trilioni na deni la ndani Sh17.3 trilioni lililotokana na kupokelewa kwa  mikopo kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.


“Taarifa ya tathmini ya uhimilivu wa deni la Serikali iliyofanyika mwaka 2020 ilionyesha kuwa deni la hilo ni himilivu kwa muda mfupi, muda wa kati na pia kwa mrefu,” amesema Dk Mwigulu.


Aidha akielezea hali ya uchumi wa nchi amesema taarifa zaidi zipo katika kitabu cha hali ya uchumi kwa mwaka 2020.


Akizungumzia mwenendo wa thamani ya shilingi dhidi ya dola za Marekani, Dk Mwigulu amesema   imeendelea kuwa tulivu.


“Dola moja ya Marekani ilibadilishwa kwa wastani wa Sh2298.5 Aprili 2021 ikilinganishwa na Sh2291.3 Aprili 2020, utulivu wa shilingi umetokana na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika usimamizi wa sera za fedha pamoja  na bajeti katika biashara ya bidhaa na huduma, lakini pia katika  uhamisho wa mali nje ya nchi na mwenendo chanya wa baadhi ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii,” amesema Dk Mwigulu.


Advertisement