Serikali ya Tanzania yaonya utoaji taarifa za maradhi, vifo

Thursday March 04 2021
serikali pic
By Peter Elias

Dar es Salaam. Msemaji mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas ametoa onyo kwa vyombo vya habari na watu binafsi kutoa taarifa za maradhi, vifo au wagonjwa bila kuzingatia misingi ya utoaji wa taarifa kwa sababu Serikali ina utaratibu wake wa kutoa taarifa.


Dk Abbas ameyasema hayo leo Alhamisi Machi 4, 2021 wakati akizungumza na Maelezo TV kuhusu tabia aliyoiona hivi karibuni ya vyombo vya habari na baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii kutoa taarifa zinazoihusu Serikali wakati kuna mamlaka husika za kufanya hivyo.


Amesema hata kwenye magonjwa ya kuambukiza na a ya mlipuko, zipo taratibu kwenye sheria za huduma ya jamii zinazoeleza ni kiongozi wa ngazi gani anapaswa kutoa taarifa kwa umma.


Advertisement

“Mtakumbuka mwaka jana Tanzania ilipopata janga la corona mheshimiwa Rais alitoa itifaki ya viongozi ambao watasemea maradhi haya ambapo ukiondoa viongozi wakuu wa kitaifa…,viongozi wengine waliopewa jukumu hilo ni Waziri wa Afya na mimi Msemaji Mkuu wa Serikali,” amesema.


Amesema baadhi ya watu wameanza kujitokeza kutoa takwimu za maradhi mbalimbali, vifo au wagonjwa kwamba hilo siyo sahihi na ameviomba vyombo vya habari kuachana na watu wa namna hiyo.


Dk Abbas amesema kila mwanajamii wakiwemo viongozi wa dini anapaswa kushiriki kwa maana ya kutoa elimu, kusisitiza hatua za kuchukua, kushiriki katika kuitoa jamii hofu na kusisitiza mambo ambayo yapo kwenye miongozo.


“Utoaji wa takwimu na masuala mengine ya kisera kwenye maeneo haya yanapaswa kubaki kwa wasemaji rasmi na wataalamu ambao wana dhamana ya kufanya hivyo,” amesema Dk Abbas.


Dk Abbas ambaye pia ni katibu mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema mpaka sasa nchi inakwenda vizuri, wamefanikiwa kuiondoa jamii hofu na watu wanafanya kazi na kushiriki burudani na maisha yanaendelea.

Advertisement