Serikali ya Tanzania yavitetea vyuo vya maendeleo

Muktasari:

  • Serikali haina mpango wa kuvifuta vyuo vya maendeleo ya wananchi na kuvifanya kuwa vyuo vya ufundi stadi (Veta) kwa kuwa bado vinahitajika

Dodoma. Serikali ya Tanzania haina mpango wa kuvibadili vyuo vya maendeleo ya wananchi kuwa Vyuo vya Ufundi Stadi (Veta). Bunge limeelezwa leo Jumatatu Juni 3,2019.

Naibu Waziri wa Elimu William Ole Nasha amesema Serikali imejikita katika kuboresha vyuo hivyo kwa kuvikarabati na kuviongezea vifaa vya kujifunza na kufundishia ili viweze kutoa mafunzo bora.

Ole Nasha amesema hayo wakati anajibu swali la mbunge wa Rufiji (CCM) Mohamed Mchengerwa ambalo liliulizwa kwa niaba yake na Mariam Kisangi (Viti Maalum-CCM).

Mbunge huyo aliuliza serikali haioni umuhimu wa kukibadili chuo cha maendeleo Ikwiriri FDC kuwa Veta ili kubadili fikra za wananchi wa Rufiji, Kibiti na Ikwiriri mkoani Pwani na hatimaye kuleta mwamko wa elimu.

Naibu Waziri amesema elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi hutolewa katika shule na vyuo katika viwango na madaraja mbalimbali kulingana na malengo yake.

Amesema vyuo vya maendeleo ya wananchi vilianzishwa kwa lengo la kumsaidia mwananchi kukabiliana na changamoto za maendeleo katika mazingira yake kwa kumpatia maarifa na stadi anuwai.

"Vyuo hivi hutoa elimu ya ufundi stadi katika hatua ya kwanza hadi ya tatu ikiwemo mafunzo ya ujasiriamali, kilimo, uvuvi na mifugo ambayo hutolewa kulingana na mahitaji ya eneo husika," amesema Ole Nasha.

Kuhusu chuo cha Ikwiriri amesema kiko kwenye orodha ya ukarabati huku akisema Rufiji ni miongoni mwa wilaya zilizotengwa fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha ufundi stadi.