Serikali yaeleza jinsi mapato sekta ya madini yatakavyofikia Sh774 bilioni kwa mwaka

Muktasari:

  • Waziri wa Madini nchini Tanzania,  Doto Biteko amesema kiwanda cha kusafisha madini cha Mwanza kitachangia sekta ya madini kufikia mapato ya Sh774 bilioni kwa mwaka.

Dar es Salaam. Waziri wa Madini nchini Tanzania,  Doto Biteko amesema kiwanda cha kusafisha madini cha Mwanza kitachangia sekta ya madini kufikia mapato ya Sh774 bilioni kwa mwaka.

 Amesema halmashauri ya Ilemela ambayo kiwanda hicho kipo itapata zaidi ya  Sh36 bilioni  na Shirika la Madini la Taifa (Stamico) litapata Sh21 bilioni kwa mwaka.

Biteko ameyasema hayo leo Jumapili Juni 13, 2021 wakati wa uzinduzi wa kiwanda hicho cha Precious Metals Refinery Limited.

Amesema kampuni 34 ziliomba  kuanzisha viwanda vya kusafisha dhahabu lakini baada ya kufanyika tathmini ya kina zikapatikana  kampuni tatu zenye  uwezo.

Amesema kiwanda hicho kina uwezo wa kusafisha kilo 480 kwa siku na kwamba baadaye kitapanuliwa kuwa na uwezo wa kusafisha kilo 960 kwa siku.

Waziri Biteko ameeleza kuwa kiwanda kingine kimejengwa Geita kina uwezo wa kusafisha kilo 400 kwa siku na kimejengwa na Mtanzania, kingine kipo Dodoma kinasafisha kilo 30 kwa siku.