Serikali yaeleza mikakati kukabiliana upungufu mafuta ya kula
Muktasari:
- Serikali imesema katika kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula nchini inatumia takribani Sh470 bilioni kuagiza tani 360,000 za mafuta ya kula nje ya nchi kila mwaka.
Dodoma. Serikali imesema katika kukabiliana na upungufu wa mafuta ya kula nchini inatumia takribani Sh470 bilioni kuagiza tani 360,000 za mafuta ya kula nje ya nchi kila mwaka.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hayo leo Jumanne Aprili 13, 2021 bungeni mjini Dodoma wakati akiwasilisha bungeni mwelekezo wa kazi za Serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya waziri mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2021/22.
Pia, amesema hivi karibuni nchi imekabiliwa na changamoto ya uzalishaji wa ndani wa mafuta ya kutosha ya kula.
Majaliwa amesema hali hiyo imetokana na uzalishaji mdogo wa mazao ya mbegu ikiwemo nazi, alizeti, pamba na chikichi.
“Kwa mfano, mahitaji ya mafuta ya kula kwa mwaka ni zaidi ya tani 570,000 wakati uzalishaji wa ndani ukikadiriwa kuwa tani 210,000,” amesema.
Amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Serikali inatekeleza mikakati ya kufufua zao la chikichi ambalo limeonekana kuwa na ufanisi mkubwa katika uzalishaji wa mafuta ya kula.
Majaliwa amesema mikakati hiyo inakwenda sambamba na kuimarisha uzalishaji kwenye mazao mengine ya mbegu ikiwemo alizeti, nazi na pamba ili kupata mafuta mengi na kujitosheleza.