Serikali yaifungulia milango China uwekezaji

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia katika kongamano la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na China.

Muktasari:

  • Kauli ya Waziri Mkuu Majaliwa imekuja wakati uwekezaji wa China ukiongezeka na kuifanya nchi hiyo kuongoza nchi zinazowekeza zaidi nchini.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema uhusiano kati ya Tanzania na China ni kichocheo cha uwekezaji, akiwataka wawekezaji kutoka nchi hiyo kuja kwa wingi kuchukua fursa.

Waziri Mkuu Majaliwa ameyasema hayo leo Septemba 25 jijini hapa alipokuwa akifunga mkutano wa uwekezaji kati ya Tanzania na China.
Kauli ya Majaliwa imekuja wakati uwekezaji wa China ukiongezeka nankuifanya nchi hiyo kuongoza nchi zinazowekeza zaidi nchini.

"Takwimu kuanzia mwaka 1997 hadi 2023 zinaonyesha China inaongeza kwa uwekezaji uliifikia zaidi ya dola 10 bilioni.
Jumla ya Miradi 1,134 ya China imesajiliwa katika kituo cha Uwekezaji (TIC) ambayo inachangia kutoa ajira nchini," amesema.

Ongezeko hilo limekuja ikiwa imepita miezi zaidi ya 10 tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipokwenda China akiwa ni rais wa kwanza wa Afrika kualikwa na nchi hiyo baada ya mkutano mkuu wa Chama cha CPC.

Ametaja uwekezaji wa nchi hiyo kuwa ni pamoja na moundombinu, usafiri, madini, kilimo, ujenzi, benki na viwanda.

"Ikumbukwe kwamba miaka 10 iliyopita China ilikuwa miongoni mwa nchi sita zilizowekeza kwa wingi Tanzania, zikiwemo Uingereza, Marekani, Afrika Kusini na Kenya.
Lakini takwimu mpya za TIC zinaonyesha China ilisogea hadi nafasi ya pili mwaka 2012 kabla ya kuongoza," amesema.

Amepongeza miradi inayotekelezwa na China akisema inatoa mchango mkubwa katika kukuza uchumi, kuzalisha ajira na kuboresha maisha ya watu.
"Sinotan ni mfano halisi ya miradi ya China kwa Tanzania," amesema.

Amesema ili kurahisisha uwekezaji, Serikali imeimarisha taratibu za uhamiaji, usajili wa biashara, vibali vyabkazi katika kituo kimoja.

Awali akizungumza katika mjadala wa uwekezaji kati ya Tanzania na China, Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo amesema ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ni wa kihistoria.

Alitaja maeneo ya ushirikiano kuwa pamoja na nchi hiyo kuliunga mkono Bara la Afrika katika kugombea ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa wakati Dk Salim Ahmed Salim (Tanzania) alipogombea.

"Tulishinda uchaguzi ule, ila mataifa ya Magharibi hayakutaka, wakatafuta mgombea asiyekuwa na upande na ndipo alipopitishwa Javier Perez De Cuellar," alisema.
Alitaja pia ujenzi wa reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) akisema uliongeza ushirikiano.
"Sio kwamba China inakuja kupora rasilimali, bali inakuja kuwekeza viwanda," alisema.

Akitaja takwimu, alisema kutoka mwakan2021 hadi 2023 nchi hiyo imewekeza dola 1.3 bilioni na imezalisha ajira 32,933.
"Agenda ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kujenga mazingira wezeshi kwa ajili ya uwekezaji wa ndani na nje, hivyo tunapoona wawekezaji kama hawa tunafurahi," alisema.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Naibu Waziri Exhaud Kigae alisema wataendelea kukuza Mpango wa Kuwezesha mazingira ya Biashara Tazania (Mkumbi) na kuhakikisha ushirikiano kati ya Tanzania na China unaendelea.

"Tutaendelea kuhakikisha tunayafikia masoko ya China na bidhaa zaonzifike maasoko yetu na ndio maana tumeona ujenzi wa kituo cha biashara cha Ubungo na tutasambaza bidhaa za China masoko ya Afrika," amesema.

Kwa upande wake Balozi wa China nchini, Chen Mingjian amesema wana imani na mikakati iliyowekwa na Tanzania.

"Tanzania yenye uchumi unaokua haraka, imeweka mikakati ya uwekezaji tangu Rais Samia Suluhu Hassan alipoingia madarajani," amesema.

Amesema Rais wa China, Xi Jinping amekuwa na mikakati ya kuliendeleza bara la Afrika kupitia uwekezaji na Tanzania ni miongoni mwa nchi zitakazonufaika.