Serikali yajivunia matunda kukitangaza Kiswahili duniani

Friday November 26 2021
kiswahili pic

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa(Bakita) Consolata Mushi akizungumza wakati wa kuwatunuku vyeti washereheshaji kwenye Ukumbi wa Utamaduni, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

By Gadi Solomon, Mwanachi

Dar es Salaam. Serikali imepongeza juhudi za ukuzaji na kueneza lugha ya Kiswahili kimataifa na hatua ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (Unesco) kutenga siku ya Kiswahili duniani.

Naibu Waziri wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Pauline Gekul amesema hayo leo Jumatano Novemba 24, 2021.

Amesema kutokana na hatua hiyo, ni muhimu matumizi ya Kiswahili yazingatie utamaduni husika.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya washereheshaji ya matumizi ya Kiswahili sanifu yaliyofanyika Ukumbi wa Utamaduni katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, amesema Unesco imekitambua Kiswahili ikiwa ni lugha ya kwanza Afrika kwa kutengewa kila Julai 7.

Naibu Waziri Gekul amesema hayo ni matokeo ya juhudi za viongozi watangulizi, pamoja na Rais Samia Hassan Suluhu kwa juhudi zake kuhimiza matumizi ya lugha ya Kiswahili nchini na kimataifa.

Advertisement

Amesema tayari kuna mipango kila kwenye ubalozi wa Tanzania kuwepo na dawati la Kiswahili ambalo litaratibu na kuwasaidia wageni wanaotaka kujifunza Kiswahili kabla ya kuja nchini.

"Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kukinadi Kiswahili, na kutafuta fursa za Kiswahili kila anapokwenda," amesema.

Amesema Watanzania wanapaswa kuwa mstari wa mbele kuzungumza Kiswahili kwani Unesco kama tayari wamekitambua, hivyo hata washereheshaji wanapaswa kukitumia bila kuchanganya na Kiingereza.

"Tusiogope kutumia lugha ya Kiswahili mbele ya wageni kwa sababu kwa kufanya hivyo tutapanua wigo kwa wakalimani nao kupata ajira," alisema Naibu Waziri.

Akizungumza wakati wa kuwatunuku vyeti vya mafunzo hayo ya siku tatu, Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita), Consolata Mushi amesema kundi hilo ni muhimu kutoa elimu ya misamiati na istilahi za Kiswahili nchini.

Alisema baraza litaendelea kupanua wigo ili mafunzo hayo yaweze kuwafikia washereheshaji wote nchi nzima.

"Bakita itaendelea kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) katika kuwadhibiti washereheshaji wasio na sifa wanaofanya kazi hizo," amesema Mushi.

 Mwenyekiti wa Chama cha Washereheshaji Tanzania, Steven Mwakajumba amesema ni wakati mwafaka sasa jamii kuwatumia washereheshaji ambao wamepatiwa mafunzo kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita).

Amesema kutokana na mafunzo ambayo Bakita imeanza kuyatoa itawapa wigo wa kufanya kazi katika maeneo mbalimbali kutokana na kutambuliwa.

Amesema Mafunzo hayo ya siku ya tatu, yamewawezesha kutambua istilahi za Kiswahili ambazo awali walitumia maneno ya Kiingereza.

Advertisement