Serikali yapewa siku 14 kurekebisha rufaa Sheria ya Vyama vya Siasa

Mawakili John Mallya na Jebra Kambole, wakizungumza na Mawakili wa Serikali katika Mahakama ya Rufaa ya Haki ya Afrika Mashariki (EACA), leo Agosti 9 2022 baada ya rufaa ya kupinga hukumu iliyotolewa na EACJ kuahirishwa. Picha na Janeth Mushi

Muktasari:

Mahakama ya Rufaa ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), imempa siku 14 Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kufanyia marekebisho nyaraka za rufaa alizowasilisha mahakamani hapo kupinga uamuzi wa mahakama hiyo ulioamuru Serikali ya Tanzania kurekebisha Sheria ya vyama vya siasa

Arusha. Mahakama ya Rufaa ya Haki ya Afrika Mashariki (EACJ), imempa siku 14 Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kufanyia marekebisho nyaraka za rufaa alizowasilisha mahakamani hapo kupinga uamuzi wa mahakama hiyo ulioamuru Serikali ya Tanzania kurekebisha Sheria yaVyama vya Siasa.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo leo Jumanne Agosti 9, 2022 baada ya kuridhika kuwa nyaraka hizo zina upungufu wa kisheria.

Katika rufaa hiyo, Serikali inapinga uamuzi uliotolewa na Mahakama ya EACJ wa Machi 25, 2022 ulioiamuru irekebisha Sheria ya Vyama vya Siasa kwa kuondoa vifungu vinavyokiuka Mkataba ulioanzisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Katika kesi ya msingi iliyompa ushindi Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, EACJ ilikubaliana na wadai kuwa sheria hiyo inakiuka vifungu vya mkataba wa kuanzishwa EAC.

Akitoa uamuzi wa mahakama hiyo leo Agosti 9, 2022 na Rais wa Mahakama hiyo, Jaji Nestor Kayobera aliyeongoza jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo, amesema rufaa hiyo ina upungufu wa kiehseia.

Mbali na Jaji Kayobera, majaji wengine wanaosikiliza rufaa hiyo namba 5/2022 ni pamoja na Jaji Sauda Mjasiri na Anitha Mugeni.

Leo shauri hilo lilifika mahakamani hapo kwa ajili ya kupanga utaratibu wa namna ya kulisikiliza ambapo pande zote wangekubaliana iwapo itasikilizwa kwa njia ya maandishi au ya mdomo.

Upande wa waleta rufaa (Jamhuri) uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Narindwa Sekimanga, Charles Mtae na Zamaradi Johanes, huku wajibu rufaa ukiwasilishwa na mawakili John Mallya, Jebra Kambole na Dito Amre.


Baada ya mahakama kuanza, Jaji Kayobera alieleza kuwa kulikuwa hakuna ukurasa unaoonyesha yaliyomo ndani ya rufaa hiyo kwenye nyaraka za rufaa zilizowasilishwa na upande wa waleta rufaa (Jamhuri).

Jaji huyo amesema kwa mujibu wa kanuni ya 99 ya uendeshaji wa mashauri wa mahakama hiyo ni muhimu iwepo ingawa kanuni 100 inaruhusu kufanyia marekebisho nyaraka endapo shauri bado halijapangiwa utaratibu wa namna ya kulisikiliza.

Baada ya maelezo ya Jaji huyo kuhusu upungufu huo, Wakili Sekimanga aliomba wafanye marekebisho hayo bila gharama na kuwa Agosti 12, watakuwa wamewasilisha upya kwa kuzingatia matakwa ya kanuni.

Jaji Kayobera aliwapa siku 14 mawakili hao wa serikali wawe wamewasilisha marekebisho hayo kwenye rufaa hiyo

Mahakama hiyo iliahirisha shauri hilo hadi Agosti 23, 2022 ambapo itapanga tarehe kuita pande zote kwa ajili ya kupanga utaratibu wa kusikiliza shauri hilo.