Serikali yaruhusu waliokatisha masomo kwa ujauzito kurejea shuleni

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ndalichako

Muktasari:

Hatimaye Serikali imeruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shuleni kwa mfumo rasmi baada ya kujifungua.

Dodoma. Hatimaye Serikali imeruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shuleni kwa mfumo rasmi baada ya kujifungua.

Pia, wanafunzi wa shule za msingi ambao wanashindwa kufaulu mitihani ya kuhitimu elimu hiyo nao watakuwa na nafasi ya kurudia mitihani kama ilivyokuwa wenzao wa vidato vya nne na tano.

Uamuzi huo umetangazwa leo Jumatano Novemba 24 2021 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ndalichako wakati akizungumzia mafanikio ya miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara.

Serikali imeruhusu wanafunzi waliokatisha masomo ikiwemo waliopata mimba Sasa wataruhusiwa kurejea shuleni baada ya kujifungua.

Akizungumza leo Novemba 24, 2021 kuhusu mafanikio ya miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Ndalichako kwa sasa kinachosubiriwa ni waraka ambao atautoa wakati wowote kuanzia leo.

"Hapa zege halilali, nitatoa waraka huo leo na hapa najaribu kutazama karatasi yangu siioni lakini kazi inaendelea leo hii nitatoa ili Watanzania wajue," amesema Profesa Ndalichako.

Kauli ya Waziri imekuja wakati kukiwa na mjadala mrefu nchini kuhusu wanafunzi waliopata mimba wakiwa shuleni wakitaka waendelee na masomo huku wengine wakigoma kwamba utaharibu mfumo wa elimu.

Wanaharakati wengi wamekuwa wakizungumzia jambo hilo tangu lilipoibuliwa kwa mara ya kwanza Bunge na aliyekuwa Mbunge wa viti Maalum Suzan Lyimo.

Leo Profesa Ndalichako amesema uamuzi huo unakwenda kutoa haki kwa wanafunzi ambao kwa sababu hizo walikuwa wamenyimwa fursa.

Kuhusu wanafunzi kurudia masomo amesema shule za Msingi walikuwa wamenyimwa haki kwani wenzao wa kidato cha nne na sita walikuwa na nafasi ya kurudia masomo pale wakishindwa kufaulu mitihani.

Hata hivyo amesema utaratibu wa kujifunza utakuwa kwa namna yao binafsi siyo katika mfumo wa Kiserikali kama inavyofanyika kwa vidato vya nne na sita.