Serikali yasema kikokotoo cha asilimia 50 hakikuwa na uhalisia

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa kupitisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jijini Dodoma leo.Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema kikokotoo cha mafao ya mkupuo cha asilimia 50 hakikuwa na uhalisia, kilikuwa na athari katika uhimilivu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.


Dodoma. Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amesema kikokotoo cha mafao ya mkupuo cha asilimia 50 hakikuwa na uhalisia, kilikuwa na athari katika uhimilivu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.

Profesa Ndalichako ameyasema hayo leo Ijumaa, Juni 24,2022 wakati akichangia mjadala wa bajeti kuu ya mwaka 2022/2023.

Amesema kanuni ya mafao ya mkupuo asilimia 33 itaanza kufanya kazi Julai 2022.

Amesema wastaafu wa sekta binafsi na mashirika ya umma waliokuwa wakipata asilimia 25 wamepandishiwa mafao yao ya mkupuo hadi asilimia 33.

 “Kanuni hizi zinakwenda kuweka kiwango sawa cha mafao kwa wafanyakazi wote, wale waliokuwa wanalipwa kidogo nao wapande,”amesema.

Amesema mstaafu aliyelipwa mafao ya mkupuo ataendelea kulipwa penshini ya kila mwezi na kutoa mfano kwa aliyelipwa Sh71 milioni ataendelea kulipwa pensheni Sh1,084,000 kila mwezi.

Profesa Ndalichakio amesema kikokotoo cha asilimia 50 kilikuwa hakina uhalisia na hivyo kusababisha kupungua kwa uhimilivu na ukwasi mwaka hadi mwaka.

Amesema Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ameeleza katika ripoti yake aliyoitoa Machi, 2022 inaonyesha gharama za mafao zinazidi makusanyo ya michango.

Amesema CAG ameonyesha kuwa katika mwaka 2020/2021 kulikuwa na tofauti kati ya makusanyo na michango ya Sh767 bilioni.