Serikali yasema maadili ya utumizi wa umma yameongezeka

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala Bora, Jenista Mhagama

Muktasari:

Serikali imesema ongezeko la kuzingatia maadili limechangiwa na Serikali kuchukua hatua za kuweka misingi imara ya usimamizi wa maadili, mazingira wezeshi na kuimarisha uwajibikaji katika utumishi wa Umma

Dodoma. Hali ya uzingatiaji wa maadili katika utumishi wa umma kwa mwaka 2022 umeongezeka kufikia asilimia 75.9 kutoka asilimia 66.9 mwaka 2014.

Taarifa hiyo imetolewa leo Desemba 9, 2022 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya utumishi wa Umma na utawala Bora, Jenista Mhagama Jijini Dodoma.

Mhagama amesema matokeo ya ongezeko la utafiti huo yamechangiwa na Serikali kuchukua hatua za kuweka misingi imara ya usimamizi wa maadili, mazingira wezeshi na kuimarisha uwajibikaji katika Utumishi wa Umma.

Hata hivyo hii ni mara ya pili kwa tafiti hiyo kubaini ongezeko hilo kwani tafiti ya kwanza mwaka 2006 ilibaini hali ya uzingatiaji wa maadili kwa watumishi wa umma ni asilimia 56.4 na kuongezeka kufikia asilimia 66.7 mwaka 2014.

Mhagama amesema utafiti huo umefanyika kwa njia ya kujibu madodoso na jumla ya sampuli za watu 1,429 walihojiwa kati yao, 793 sawa na asilimia 55.5 ni wanaume, 636 sawa na asilimia 44.5 ni wanawake.

“Aidha katika kuhakikisha dhana ya usawa inazingatiwa katika dodoso hilo wahojiwa 700 (asilimia 49) walikuwa watumishi wa umma na 729 sawa na asilimia 51 walikuwa wananchi wasio watumishi wa umma,” amesema.