Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Serikali yashauriwa kuongeza Maofisa Ustawi Jamii

Mwanga. Kamati ya kudumu ya Bunge ya ustawi na Maendeleo ya jamii imeishauri serikali kuongeza Maofisa ustawi wa jamii katika maeneo mbalimbali nchini ili kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyofanywa na baadhi ya wanajamii na kujeruhi mioyo ya Watanzania.

Imesema kwasasa kumekuwepo na mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii hali ambayo imepelekea watu kuuana, kutesana, kujeruhiana na kujengeana chuki zisizoisha kwenye jamii.

Kamati hiyo ya Bunge ilitembelea jana Taasisi ya ustawi wa jamii kampasi ya Kisangara, wilayani Mwanga, mkoani Kilimanjaro kujionea shughuli mbalimbali za ujenzi wa miundo mbinu ya hosteli na Madarasa inayoendelea katika Taasisi hiyo.

Akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya mradi wa ujenzi wa miundo mbinu katika Taasisi hiyo, Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma za ustawi na Maendeleo ya jamii, Fatma Tawfiq alisema kumekuwepo na mmomonyoko mkubwa wa maadili katika jamii hivyo akaishauri serikali kuongeza Maofisa ustawi wa jamii ili waweze kutibu mioyo ya watu ambayo imejeruhiwa.


"Tumekuja, tumeona kazi nzuri inayofanywa na uongozi wa chuo hiki, hongereni sana uongozi wa chuo, fedha zenu za ndani ambazo zinapatikana kutokana na ada za wanafunzi mmeweza kutumia kikamilifu na baadhi ya miundo mbinu mmejenga kwa kutumia hizi fedha za ndani, "

Pamoja na idadi hiyo ya wanafunzi kuongezeka alisema hali ya maadili iliyopo kwasasa nchi inahitaji kuwa na matabibu wa mioyo ya watu ambao wamepata madhila.

"Hali ya maadili tunayoiona kwa sasa tunahitaji matabibu wa mioyo, tunaona matatizo ya mauaji yamekuwa ni mengi, watu kuuana, kufanyiwa ukatili wa aina tofauti tofauti hivyo, tunahitaji sana Maofisa ustawi ili kusudi wakatibu Ile mioyo ya Watanzania ambao kwa njia moja au nyingine ina madhila makubwa, "

"Hili jambo la kuweza kuwa na hawa matabibu tunahitaji sana katika jamii zetu, maana hapa katikati kuna ombwe limetokea, sijui limetokea wapi, kwa hiyo ni vizuri tukawa na hawa watu kwenye vituo vyetu, ili watu waende na kama mtu kama ana mambo yake mazito na madhila yaliyomsonga kwenye moyo akifika anaweza akazungumza na akapewa utabibu wa moyo,"


Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum Dk. Dorothy Gwajima alisema chuo hicho kitaendelea kuboresha miundo mbinu ya kufundishia ili kuweza kuzalisha wataalam wengi katika taaluma ya ustawi wa jamii ambao watakuwa ni msaada mkubwa kwa Taifa.

Dk.Gwajima alisema chuo hicho kimekuwa na mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake ambapo idadi ya wanafunzi imeweza kuongezeka kutoka wanafunzi 56 mwaka 2016/17 hadi kufukia wanafunzi 245 mwaka 2022/23 sawa na ongezeko la asimilia 337.


Pamoja na mambo mengine, alisema wanaandaa mtaala wa Elimu ya malezi na makuzi ya awali ya watoto katika ngazi ya cheti hadi ngazi ya stashahada na tayari umeidhinishwa kwa matumizi na Mamlaka ya Elimu ya ufundi na Ufundi stadium (Nactevet).

Mwenyekiti wa Bodi ya Magavana wa Taasisi ya Ustawi wa jamii nchini, Sophia Simba aliishukuru kamati hiyo kwa kukitembelea chuo hicho na kueleza mawazo yaliyotolewa na wabunge hao watayafanyia kazi.


"Namshukuru Waziri Gwajima kwa kukipendelea sana hiki chuo, tunashukuru sana kwa michango yenu kamati ya Bunge iliyofika hapa, tutachukua mawazo yenu mliyotoa na kuyafanyia kazi.


Naye, Katibu Mkuu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wanawake na Makundi Maalum, John Jingu alisema watahakikisha mitaala inayotolewa katika chuo hicho, inazingatia utamaduni, Mila na desturi za hapa nchini lakini mahitaji ambayo nchi inahitaji kulingana na mazingira yaliyopo.