Serikali yasisitiza wamachinga waondolewe kwa utaratibu

Tanzania kupokea chanjo 500,000 za Pfizer mwisho wa Oktoba

Muktasari:

  • Kutokana na kuwapo kwa malalamiko ya matumizi ya nguvu katika kuwahamaisha wamachinga, Serikali imesisitiza kwamba wafanyabiashara hao wadogo wanatakiwa kuondolewa kwa utaratibu.

Mwanza. Zikiwa zimepita siku 17 tangu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Selemani Sekiete atoe agizo kwa wamachinga kuondoka kwa hiari na kwenda maeneo yaliyoelekezwa, Serikali imesisitiza kwamba ilitoa maelekezo kwa viongozi wa halmashauri zote nchini kuwahamisha na kuwapanga wafanyabiashara hao kwa utaratibu.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza leo, Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msingwa amesema miongoni mwa vigezo vinavyotakiwa kuzingatiwa katika kuwahamisha wafanyabiashara hao ni kuwapeleka katika maeneo yenye huduma za msingi vikiwamo vyoo, maji na yanayofikika kwa urahisi na wateja.

Awali, mmoja wa waandishi wa habari alihoji kuhusu malalamiko ya kutumia nguvu kuwahamisha wamachinga kutoka maeneo hatarishi jijini humo.

"Kuna machinga wanadai wamevunjiwa vibanda vyao kabla hawajaondoa mali zao, wengine wamelalamika kupigwa na watu wanaowahamisha, je, huo ndio msimamo wa Serikali?" alihoji mwandishi huyo.

Akijibu tuhuma hizo, Msigwa amesema hayo siyo maelekezo ya Serikali inayotaka kuwaondoa na kuwapanga kwa utaratibu ikiwamo kuwapeleka maeneo ambayo ni rasmi, yenye huduma za msingi na yanayoweza kufikika kwa urahisi na wateja.

"Kama kuna malalamiko ya watu kupigwa hilo ninalichukua ili nilifanyie kazi, nitazungumza na mkuu wa mkoa ili tuweze kulitatua," amesema Msigwa