Serikali yasitisha bei mpya za vifurushi

Friday April 02 2021
bando pichaa
By Mwandishi Wetu

Dar es Salaam. Saa chache baada ya kutangazwa kwa bei mpya za vifurushi, Serikali imetangaza kusitisha kutumika kwa gharama hizo hadi hapo itakapotangazwa baadaye.

Uamuzi huo unaweza kuwa habari njema kwa watumiaji wa mitandao ya simu ambao, tangu kutangazwa kwa bei hizo mpya mapema leo Ijumaa ya Aprili 2, 2021, wamekuwa kwenye mjadala mzito kwani, matarajio ya wengi ilikuwa ni kushuka kwa gharama hizo.

Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Semu Mwakyanjala, amesema matumizi ya bei mpya ya vifurushi yamesitishwa kwa muda.

Hata hivyo, amesema uamuzi huo utahusu vifurushi vya data pekee huku vile vya ujumbe mfupi wa maneno na kupiga zitaendelea kama ilivyotangazwa mapema leo Ijumaa.

“Tumesitisha matumizi ya gharama mpya za vifurushi hadi hapo itakapotangazwa baadaye. Lakini, hili litahusu vifurushi vya data pekee na vile vya sms na kupiga vitaendelea kama kawaida,” amesema Mwakyanjala alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu dakika chache zilizopita.

Kanuni ndogo za gharama na tozo za vifurushi, utangazaji wa huduma na ofa maalum zilizotungwa na TCRA, zimeanza kutumika leo ambapo, matumaini ya wengi ilikuwa ni bei za vifurushi kupungua lakini ikawa tofauti.

Advertisement

Mwanzoni mwa Machi, 2021 Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba aliahidi utekelezaji wa kanuni hizo za kukabiliana na malalamiko juu ya huduma ya vifurushi yaliyotokana na maoni 3, 278 yaliyotolewa na wananchi.

Baadhi ya changamoto ambazo watumiaji wa huduma za simu walikuwa wakikutana nazo na kuzilalamikia ni pamoja na gharama za vifurushi kuwa juu na vifurushi vya data kubadilika mara kwa mara.

Jana mitandao ya simu iliwataarifu watumiaji wake juu ya mabadiliko hayo, lakini jambo ambalo limewaibua wengi hususani katika mitandao ya kijamii ni kuminywa kwa vifurushi hivyo kuliko hata ilivyokuwa awali wakati wanatoa malalamiko hayo.

Katika makundi ya mtandao wa kijamii wa WhatsApp na mitandao mingine ya kijamii inayokutanisha watu kama Twitter, Instagram na Facebook mjadala ni vifurushi ambavyo vimebadilika katika mitandao yote ya huduma za simu wengi wanaomba walau hali irudi kama ilivyokuwa.

Mitandao mbali ya simu kama ilivyo ada katika sikukuu mbalimbali ilituma salamu zao za sikukuu kupitia kurusa zao za mitandao ya kijamii, lakini maoni ya wananchi wengi si kupokea salamu hizo bali ilikuwa ni kulalamikia mabadiliko yaliyofanywa katika vifurushi.


Advertisement