Serikali yasitisha uchinjaji punda

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023, jijini Dodoma leo. Ndaki ameliomba bunge lipitishe bajeti ya wizara hiyo kiasi cha Sh286 bilioni.  Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

Serikali imesitisha shughuli zote za biashara ya uchinjaji wa punda nchini kutokana na kupungua kwa idadi ya wanyama hao.

Dodoma. Serikali imesitisha shughuli zote za biashara ya uchinjaji wa punda nchini kutokana na kupungua kwa idadi ya wanyama hao.

 Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema hayo leo Jumatano Mei 25, 2022 wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2022/2023.

Mashimba amesema kutokana na kupungua kwa idadi ya punda nchini na hatari ya kutoweka kwa kizazi cha punda ambapo katika mwaka wa fedha 2021/2022 idadi ya punda ni takriban 650,000,

“Napenda kutumia fursa hii kuwataarifu wawekezaji waliowekeza katika machinjio za punda nchini watumie miundombinu ya machinjio hizo kwa ajili ya kuchinja na kuchakata aina nyingine za mifugo hususani ng’ombe, mbuzi na kondoo,”amesema.

Aidha, Mashimba amesema matukio ya ukamataji na utaifishaji wa mifugo usiofuata utaratibu hususani kwenye maeneo ya hifadhi yamepungua kutoka mifugo 6,245,356 iliyokamatwa mwaka 2020/2021 hadi mifugo 3,343 iliyokamatwa mwaka 2021/2022.

Amesema hiyo imetokana na wadau mbalimbali kuelewa Sheria ya Ustawi wa na kanuni ya Animal Welfare pamoja na sheria nyingine za nchi.